
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amekejeli na kukosoa vikali tafsiri ya Marekani ya ‘diplomasia’ katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisisitiza kuwa, uwazi na utayarifu kwa mazungumzo hauna mfungamano wowote na kuuripua kwa mabomu upande wa pili wakati wa majadiliano.
Morgan Ortagus, Naibu Mjumbe Maalum wa Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia, aliliambia Baraza la Usalama siku ya Jumanne kwamba, Washington ingali tayari kwa mazungumzo “ya maana” na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia, lakini akasema eti utawala wa Rais Donald Trump hautaruhusu kurutubishwa urani katika ardhi ya Iran.
Akijibu bwabwaja hizo, Araghchi ameyaelezea matamshi hayo kama “fasili mpya ya diplomasia ya Marekani.” Akiashiria kuwa Washington inataka kukanyaga “haki zinazotambulika kimataifa” za Tehran za kurutubisha urani, Waziri Araghchi amesema kuwa, “Hii ni amri na sio mazungumzo, achilia mbali (kuwa mazungumzo) ya maana.”
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amefafanua kwenye ujumbe wake huo alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa, “Ulimwengu ulishuhudia jinsi tulivyokuwa kwenye mazungumzo, wakati Marekani ilipokhitari kuwavurumishia (mabomu) watu wetu na kuvuruga diplomasia.”
Araghchi amesema hayo akirejelea uchokozi wa Israel na Marekani dhidi ya nchi hii mwezi Juni mwaka huu na kuongeza kuwa, “Tulifanya kile tunachofanya kila wakati: kupinga na kukabiliana na wale wanaotushambulia, na kuhakikisha wanajuta.”
Ikiungwa mkono na Marekani, Israel ilianzisha chokochoko dhidi ya Iran mnamo Juni 13, siku chache kabla ya duru ya sita ya mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington. Tarehe 24 Juni, Iran, kupitia operesheni zake za kulipiza kisasi zilizofanikiwa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani, iliweza kusimamisha mashambulizi hayo haramu.