
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limekamata meli iliyokuwa imebeba shehena kubwa ya mafuta ya magendo katika maji ya Ghuba ya Uajemi.
Tovuti ya habari ya IRGC iliripoti jana Jumatano kwamba, meli hiyo ilikuwa na lita milioni 4 za mafuta ya magendo ilipokamatwa katika maji ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kamanda wa Kikosi cha Kwanza cha Jeshi la Wanamaji la IRGC, Brigedia Jenerali Abbas Gholamshahi, amesema kuwa wafanyakazi 16 waliokuwa kwenye meli hiyo, wote wakiwa raia wa kigeni, wanazuiliwa baada ya kukamatwa wakati wa operesheni hiyo.
Kikosi cha Wanamaji cha IRGC kimebainisha katika taarifa hiyo kwamba, “operesheni hiyo ilifanyika kwa kuzingatia majukumu ya kisheria na kwa ajili ya kulinda maslahi ya taifa na rasilimali za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.” Taarifa ya kikosi hicho cha Wanamaji cha IRGC imebainisha kuwa meli hiyo, shehena yake, na nyaraka zake zilichunguzwa kikamilifu, na kwamba meli hiyo imepatikana na hatia ya “kubeba shehena isiyo na kibali.”
Hivi karibuni pia, Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) kilikamata meli nyingine ya mafuta katika pwani ya kusini ya Makran baada ya kupokea amri ya mahakama.
Taarifa ya ofisi hiyo ilisema kuwa, meli hiyo ya mafuta, ikiwa imebeba tani 30,000 za vifaa na mada za petrokemikali na ikiwa njiani kuelekea Singapore, iliongozwa kutia nanga kwa ajili ya uchunguzi kuhusiana na ukiukaji iliofanya.
Usafirishaji wa mafuta kwa njia ya magendo ni changamoto inayoendelea kuikumba Iran; magendo ambayo yanamaliza rasilimali za taifa na kudhoofisha uthabiti wa kiuchumi wa Jamhuri ya Kiislamu. Tehran imesisitiza azma yake ya kulinda rasilimali zake za nishati na kudhibiti shughuli za baharini katika Ghuba ya Uajemi, eneo ambalo tayari linashuhudia mvutano wa kijiografia.