
Kuishi chini ya kipato chako, sio ndani ya kipato chako ni nidhamu inayojenga uhuru wa kifedha katika kipindi ambacho gharama za maisha zinaongezeka, shinikizo la kijamii ni kubwa na mikopo inapatikana kirahisi.
Haya yote hutokea wakati ambao watu wengi hujivunia kusema wanaishi ndani ya kipato chao ingawa kauli hii inaonekana ya uwajibikaji lakini mara nyingi haitoshi.
Ustawi wa kweli wa kifedha hujengwa kwa kuishi chini ya kipato chako, sio tu ndani ya kipato chako, haya mawili tofauti yake ni ndogo lakini nguvu yake ni kubwa.
Kuishi ndani ya kipato chako maana yake ni kutumia mapato yako yote bila kuingia kwenye madeni. Kipato kinaingia, matumizi yanatoka na mwisho wa mwezi salio linakaribia sifuri nah apo ndiyo bili zinalipwa lakini hakuna akiba ya maana kwa ajili ya baadaye.
Njia hii inaweza kukuweka salama leo lakini inakuacha hatarini kesho. Mshtuko wowote kama ugonjwa, kupoteza kazi, ada za shule au kupanda kwa bei unaweza kukusukuma haraka kuingia kwenye madeni na msongo wa mawazo ya kifedha. Kuishi chini ya kipato chako kwa upande mwingine ni uamuzi wa makusudi, inamaanisha kutumia chini ya unachopata na kuweka akiba au kuwekeza tofauti hiyo mara kwa mara.
Tabia hii hutengeneza nafasi ya kupumua kifedha, inakupa chaguo, uimara na amani ya moyo na hiyo inakufanya usiishi tu bali unajiandaa kwa maisha ya baadaye.
Moja ya vikwazo vikubwa vya kuishi chini ya kipato chako ni matumizi yasiyo ya lazima. Matumizi mengi huingia kimya kimya, kula hotelini au mgahawani mara kwa mara, manunuzi ya pupa, kubadili simu au gari mara kwa mara au ada za huduma tusizotumia na maamuzi ya maisha yanayoongozwa na kulinganisha na wengine badala ya uhitaji halisi.
Kila moja linaweza kuonekana dogo lakini yakikusanyika, huondoa kipato ambacho kingejenga akiba au uwekezaji.
Kuepuka matumizi yasiyo ya lazima haimaanishi kuishi maisha ya mateso au kujinyima kila kitu bali inamaanisha kujifunza kutofautisha kati ya mahitaji, matakwa na anasa.
Mahitaji ni ya lazima kama chakula, makazi, mavazi ya msingi, usafiri, afya, na elimu lakini matakwa huongeza faraja lakini si ya lazima. Anasa ni vitu vya hiari vinavyopaswa kufurahiwa tu baada ya akiba na uwekezaji kuwa salama.
Njia rahisi ni kutumia mpangilio wa matumizi, tanguliza mahitaji muhimu kwanza, tenga sehemu ya akiba na uwekezaji mara moja, kisha tumia kilichobaki kwa matumizi ya hiari. Akiba isiwe kile kinachobaki mwisho wa mwezi bali itazamwe kama gharama ya lazima kwa ajili ya nafsi yako ya baadaye.
Kuishi chini ya kipato chako pia hukulinda dhidi ya mtego wa kuongezeka kwa mtindo wa maisha. Kipato kinapoongezeka watu wengi huongeza matumizi bila kuongeza akiba kwa kasi ile ile na matokeo yake ni kufanya kazi zaidi lakini kujisikia salama kwa kiwango kilekile.
Historia na uzoefu vinaonyesha kuwa watu wanaoishi chini ya kipato chao hujenga utajiri polepole lakini kwa uhakika, ilhali wale wanaoonekana “wanaishi maisha makubwa” mara nyingi hupambana kwa siri na madeni na wasiwasi.
Mafanikio ya kifedha hayapigi kelele ni ya subira, ya uthabiti na ya nidhamu, kuishi ndani ya kipato chako hukulinda leo lakini kuishi chini ya kipato chako hulinda kesho yako.
Epuka matumizi yasiyo ya lazima, chelewesha kuridhika na fanya maamuzi ya kifedha kwa makusudi. Kesho yako itakushukuru kwa nidhamu unayojifunza leo.