RAIS wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, amezindua rasmi Uwanja wa Hoima City wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000, sehemu ya maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, litakaloandaliwa kwa pamoja na Uganda, Kenya na Tanzania.
Uzinduzi huo haukuwa wa hotuba tu. Rais Museveni aliwashangaza wananchi na wageni baada ya kuchukua mpira wa miguu na kuanza kuubutua juu, akipiga danadana kadhaa katikati ya uwanja. Tukio hilo lilizua shangwe na vicheko, huku wengi wakishangaa akisema, “Kumbe bado yumo eh!” licha ya umri wake. SOMA:Samia: Nimemuenzi Magufuli

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Museveni alisema maendeleo yanayoendelea nchini Uganda ni matokeo ya sera za kimapinduzi, akitolea mfano mafanikio ya kampuni ya Kira EV inayotengeneza mabasi ya umeme, ambayo tayari imepokea oda ya mabasi 450 hadi Afrika Kusini.
Rais pia alisema Uwanja wa Hoima City ni mojawapo ya miradi 10 ya kimkakati inayotekelezwa kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027, akipongeza kampuni ya Kituruki Summa kwa kazi nzuri ya ujenzi na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika miradi mingine ya maendeleo.
