Papa Leo XIV ametoa baraka yake ya kwanza ya Krismasi kutoka Kanisa la Mtakatifu Petro Alhamisi, akilaani hadharani hali wanayoishi Wapalestina huko Gaza, katika hotuba isiyo ya kawaida kwa ibada ambayo kwa kawaida huwa ya kiroho na tulivu.
Katika mahubiri yake, Papa alisema simulizi la Yesu kuzaliwa zizini linaonyesha kuwa Mungu “alipiga hema lake dhaifu” miongoni mwa wanadamu, akirejelea mahema ya wakazi wa Gaza ambao kwa wiki kadhaa wamekuwa wakikabiliana na mvua, upepo na baridi kali. Alisema haiwezekani kusherehekea Krismasi bila kuwakumbuka watu wanaoishi katika mateso makubwa.
Hata hivyo, wito wa Papa wa kusitisha mapigano duniani kwa siku moja haukuzingatiwa nchini Ukraine, ambako mapigano yaliendelea, wakati akijiandaa kutoa baraka ya Urbi et Orbi majira ya mchana, ambapo kwa kawaida mapapa huzungumzia migogoro duniani na kutoa wito wa amani.
Papa Leo, aliyeteuliwa Mei kuchukua nafasi ya hayati Francis, anajulikana kwa mtindo wa utulivu na wa kidiplomasia, na kwa kawaida huepuka lugha ya kisiasa.
Hata hivyo, katika wiki za karibuni amekuwa akilalamikia mara kwa mara hali ya Gaza, akisema suluhu ya mgogoro wa muda mrefu kati ya Israel na Wapalestina lazima ihusishe kuundwa kwa taifa la Palestina.
Katika ibada iliyofanyika mbele ya maelfu ya waumini ndani ya Kanisa la Mtakatifu Petro, Papa pia alilaani mateso ya watu wasio na makazi duniani na uharibifu unaosababishwa na vita, akisema miili na maisha ya raia wasio na ulinzi, hususan vijana wanaolazimishwa kubeba silaha, ni dhaifu na huachwa na majeraha ya kudumu.
Papa Leo pia ataongoza misa nyingine Siku ya Krismasi, akifufua utamaduni uliokuwepo wakati wa marehemu John Paul II.
Sherehe Bethlehem
Huko Bethlehem, jumuiya ya Wakristo ilisherehekea Krismasi ya kwanza yenye shamrashamra katika zaidi ya miaka miwili, baada ya mji huo wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu kuanza kutoka kwenye kivuli cha vita vya Gaza.
Katika kipindi chote cha mzozo ulioanza baada ya shambulio la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 2023, Krismasi mjini Bethlehem—mahali pa kibiblia pa kuzaliwa Yesu Kristo—imekuwa na hali ya huzuni. Lakini Jumatano, sherehe zilirejea kwa gwaride na muziki, wakati usitishaji dhaifu wa mapigano ukiendelea Gaza.
Mamia ya waumini walikusanyika kwa ibada ya Misa katika Kanisa la Kuzaliwa kwa Yesu. Viti vilijaa kabla ya usiku wa manane, na waumini wengi walisimama au kukaa sakafuni kufuatilia misa ya jadi ya kuikaribisha Siku ya Krismasi.
Saa 11:15 jioni muziki wa organa ulisikika huku msafara wa makasisi kadhaa ukiingia, ukifuatiwa na Patriarki wa Kilatini wa Jerusalemu, Kardinali Pierbattista Pizzaballa, aliyewabariki waumini kwa ishara ya msalaba.
Katika mahubiri yake, Pizzaballa alitoa wito wa amani, matumaini na kufufuka upya, akisema simulizi la Kuzaliwa kwa Yesu bado lina umuhimu katika nyakati za sasa. Alisema licha ya kusitishwa kwa mapigano, mateso bado yanaendelea Gaza, lakini alisifu nguvu ya watu na hamu yao ya kuanza upya.
“Yajaa furaha”
Mamia ya watu walishiriki maandamano kupitia Mtaa wa Star mjini Bethlehem, huku umati mkubwa ukikusanyika Uwanja wa Manger. Milagros Anstas, 17, alisema siku hiyo ilikuwa ya furaha kwa kuwa kwa muda mrefu sherehe zilikuwa zimesitishwa kutokana na vita.
Taa za rangi mbalimbali ziliangaza uwanja huo jioni, huku mti mkubwa wa Krismasi uking’aa karibu na Kanisa la Kuzaliwa kwa Yesu. Wakazi walisema kurejea kwa sherehe kunatoa matumaini ya kuufufua tena mji huo. George Hanna kutoka Beit Jala alisema ujumbe wa furaha unapaswa kuifikia dunia nzima.
Nchini Syria, taa za Krismasi ziliangaza Mji wa Kale wa Damascus licha ya hofu ya vurugu baada ya shambulio la mauaji mwezi Juni. Mwanafunzi Loris Aasaf, 20, alisema Syria inastahili furaha na matumaini ya mustakabali mpya.
Sherehe zenye huzuni
Kinyume na ujumbe wa viongozi wa kidini, Rais wa Marekani Donald Trump alitoa salamu za Krismasi kwa “kila mtu, wakiwemo wanamrengo mkali wa kushoto,” akiwalenga chama cha Democratic.
Hali mbaya ya hewa pia ilivuruga msimu wa sikukuu nchini Marekani, hasa jimboni California, ambako mamlaka zilitangaza hali ya hatari katika Los Angeles kwa hofu ya mafuriko.
Nchini Australia, Waziri Mkuu Anthony Albanese alitoa ujumbe wa huzuni kufuatia shambulio lililosababisha vifo wakati wa sherehe za Hanukkah katika Ufukwe wa Bondi Desemba 14, akisema taifa lilihisi uzito wa majonzi baada ya tukio hilo.
Chanzo: AFP, RTRE