
Kiongozi huyo wa Kamati ya Sera ya Nje ya Bunge la Ujerumani, Armin Laschet amesisitiza kuwa Ulaya inapaswa kuwa na sera yake imara ya kigeni na usalama, inayojitegemea na yenye mamlaka kamili bila kutegemea wapatanishi wa Marekani.
Laschet amesema mpango wa amani wa Ulaya unaokubaliwa na Ukraine unahitajika ili uwasilishwe kwa Urusi kutokea kwenye nafasi ya nguvu. Ameongeza kuwa kutumia wajumbe wa Marekani kama Steve Witkoff au Jared Kushner kuwasilisha ujumbe kwa Moscow hakudhihirishi kujiamini wala uhuru wa Ulaya.
Amesema juhudi zozote za mazungumzo na Vladimir Putin zinapaswa kuongozwa kwa pamoja na Berlin na Paris, akibainisha kuwa bila Ujerumani na Ufaransa, Ulaya haiwezi kujengwa. Kauli hiyo inakuja baada ya Emmanuel Macron kusema mazungumzo ya moja kwa moja na Urusiyanaweza kuwa muhimu, huku Rais Vladmir Putin akionyesha utayari wa kuzungumza na Ufaransa.