Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya malipo ya kielektroniki, hali inayodhihirisha mageuzi makubwa ya sekta ya fedha na biashara.

Kuenea kwa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, huduma za kibenki kwa njia ya kidijitali na mifumo ya malipo ya papo hapo kumeleta urahisi, usalama na ufanisi katika kufanya miamala ya kifedha kwa wananchi na taasisi mbalimbali.

Ukuaji huu umechangiwa na ongezeko la matumizi ya simu janja, upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano, pamoja na juhudi za Serikali na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika kuimarisha mifumo ya malipo na sera jumuishi za kifedha.

Ripoti ya Monetary Policy ya BoT ya Oktoba mwaka huu, inaonyesha kuwa mifumo ya malipo iliendelea kufanya kazi kwa ufanisi huku ikiwezesha ulipaji mzuri wa miamala ya kifedha, kuimarisha uthabiti wa kifedha, na kusaidia utekelezaji bora wa sera ya fedha.

Hali hiyo ilifanya kiasi cha miamala kuongezeka katika mifumo yote ya malipo hususan ya fedha  iliyopitia mfumo wa malipo makubwa na ya haraka (TISS) iliyofikia Sh31.1 trilioni katika mwaka ulioishia Agosti mwaka huu kutoka Sh29 trilioni Agosti 2024.

Miamala ya fedha kwa njia ya simu ilifikia Sh23 trilioni ikilinganishwa na Sh18 trilioni Julai 2024, huku miamala iliyofanyika kupitia Mfumo wa Malipo ya papo hapo (TIPS) ikiongezeka hadi Sh4.9 trilioni kutoka Sh2.7 trilioni Agosti 2024.

Ripoti hii inabainisha kuwa ongezeko kubwa la miamala ya TIPS lilichangiwa na kupanuka kwa matumizi yake, ikiwamo malipo kwa taasisi za serikali na kuongezeka kwa matumizi ya malipo ya wafanyabiashara yanayoweza kufanyika kwa mwingiliano wa mifumo.

Hiyo ilitokana na juhudi zinazofanywa na BoT katika kushughulikia vikwazo vya huduma za kifedha za kidijitali, kama vile mapitio ya ada za miamala ya malipo ya TIPS ambazo zilichangia kuongezeka kwa mahitaji ya huduma hizi.

“Pia miamala ya fedha za simu ilinufaika na mazingira mazuri ya mfumo wa malipo yaliyojengwa na ada nafuu, imani ya watumiaji na miundombinu ya kidijitali iliyo imara,” imeeleza ripoti hiyo.

Nini maana yake

Akizungumzia ukuaji huu, Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Yohana Lawi amesema kuongezeka kwa malipo ya kidigitali ni njia sahihi ambayo serikali inaweza kukusanya mapato yake bila kupoteza na kuwa na uwezo wa kudhibiti kinachoingia.

Amesema licha ya kuonekana kuongezeka lakini malipo ya kielektroniki bado yapo chini hivyo elimu zaidi inahitajika kutolewa kwa watu mbalimbali ikiwamo wafanyabiashara na wananchi ili waweze kutambua manufaa yake.

“Kwenye nchi za wenzetu unapofanya malipo kielektroniki unapata punguzo kidogo la huduma tofauti na anayetumia fedha taslimu, inafanya anayehudumiwa atamani kutumia zaidi njia ya kielektroniki kwa sababu kuna motisha huko,” anasema.

Anasema wamefanya hivyo ili kuvutia watu kutumia njia za malipo za kielektroniki zaidi jambo linaloongeza makusanyo ya serikali kwa urahisi kwani kodi inakatwa moja kwa moja.

“Kwa wenzetu hata kama hauna simu na uko baa kuna njia inayokuwezesha kulipa kielektroniki, hata mgahawani malipo yanafanyika, matumizi ya fedha taslimu katika dunia ya kwanza ni kama hayapo kwani utanunua kwa gharama zaidi na wengine hawapokei fedha taslimu kabisa,” anasema.

Hilo limeenda mbali hadi kwenye vitu vya usafiri jambo ambalo linapaswa kuigwa na Tanzania ikiwa inataka kuachana na matumizi ya fedha taslimu.

“Serikali iweke vivutio haiwezekani ninayelipa kielektroniki nitoe sawa na anayelipa fedha taslimu kwa sababu ninakatwa lakini tukumbuke kuwa kutumia fedha taslimu pia fedha zinaharibika kuzitengeneza kuna gharama nyingine,” anasema.

Anasema licha ya mafanikio yanayoonekana lakini sehemu nyingi bado zina matumizi ya fedha taslimu kuliko matumizi ya kielektoniki hivyo jitihada zaidi zinahitajika.

“Tunataka hii iende kote katika masoko, bodaboda, kila mtu afanye miamala kwa kutumia njia za kielektoniki tukifika hapo tutakuwa tumeisaidia serikali kufanya makusanyo kwa njia rahisi,” anasema Dk Lawi.

Mtaalamu wa uchumi, Dk Goodhope Mkaro anasema kukua kwa malipo ya kielektroniki pia ni ishara ya ukuaji wa ujumuishaji wa huduma za kifedha hasa kupitia matumizi ya simu za mkononi.

Hiyo ni kwa sababu kutumia simu kupata huduma za kifedha inaweka wigo mpana zaidi na kuwafikia watu mbalimbali hata ambao wanaishi sehemu ambazo hakuna benki kama vijijini.

“Hii inasaidia ujumuishaji hadi katika sehemu ambazo hakuna benki na simu za mkononi ndiyo inakuwa suluhisho. Pia hii ni ishara kuwa elimu ya fedha inaongezeka na watu wanaacha kutembea taslimu, wanaweka katika simu, wanaweka benki wameacha kuhifadhi fedha kwenye magodoro na wengine wanaweka akiba,” anasema.

Anasema watoa huduma ikiwamo wafanyabiashara kutambua maana ya malipo ya kielektroniki nayo ni moja ya sababu ya kukua kwa malipo haya kwani wameweka njia mbalimbali za malipo ikiwamo ‘QR Codes’ ambazo zinawezesha watu kulipa kirahisi.

“Sasa kadri kunapokuwa na urahisi wa kufanya miamala inakuwa rahisi pia kupata huduma, manunuzi yanafanyika kirahisi na uuzaji pia hii inafanya uchumi unazidi kukua kwa sababu miamala inakuwa mingi,” anasema.

Wafanyabiashara wanena

Wakati wataalamu wa uchumi wakiyasema hayo wafanyabiashara nao wameeleza namna malipo ya kielektroniki yalivyorahisisha shughuli zao za kila siku.

Akizungumzia huduma hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa mabasi ya Buti la Zungu, Saidi Machokole anasema malipo ya huduma kielektroniki yamekuwa ni salama zaidi katika shughuli zake za kila siku kwa sababu hapokei pesa nyingi taslimu kutoka kwa makondakta.

“Kwa mfano, malipo ya tiketi za safari huingia moja kwa moja kwenye akaunti ya kampuni hii inapunguza hatari ya wizi au upotevu wa fedha na inaniwezesha kupokea malipo muda wote ndani ya saa 24,” anasema.

Anasema hiyo pia inampa abiria uhakika wa safari kwani anaweza kulipia tiketi yake usiku au mapema asubuhi kabla ya safari jambo linalorahisisha mipango yake.

“Pia ni rahisi kwangu kufuatilia mapato ya kampuni, naweza kuona ni basi lipi limeuza tiketi nyingi kwa siku au wiki kupitia rekodi za malipo ya kidijitali,” anasema Machokole ambaye anakiri kuwa wateja wengi sasa wanakata tiketi zao kwa njia ya kielektoniki kupitia simu zao za mkononi.

Maneno yake yaliungwa mkono na Amin Alawi ambaye ni mfanyabiashara wa vipodozi anayesema malipo ya kielektroniki yameongeza ufanisi katika viashara yake ya jumla na rejareja.

“Mteja wa jumla anaponunua manukato, mafuta ya nywele huweza kulipa kwa M-Pesa au benki na mimi hupokea fedha papo hapo. Mfumo huu umenirahisishia kulipa bili na huduma mbalimbali,” anasema.

Anasema uwepo wake umarahisisha hata ufanyaji biashara na watu walio mbali huku ikiondoa ulazima wa wateja kufika dukani kufuata mizigo na badala yake hufanya malipo ya kile wanachohitaji na wao kutumiwa bidhaa hadi sehemu walipo. “Pia ni salama sana kwani badala ya kujaza fedha dukani nyingi inakuwa ipo katika akaunti ya benki au laini za simu, inakuondolea mawazo ya kufikiria nini kitatokea,” anasema.

Wakati wakiyasema hayo, wateja wao wanaomba kuendelea kuwekwa ahueni Zaidi ili waone faida ya kutumia malipo ya kielektroniki badala ya fedha taslimu.

“Tunapolipia huduma basi makato yapunguzwe, hii itavuta wengi, isijekuwa mtu anaona kulipa Sh50,000 atahitaji labda na Sh4,000 ya makato anaona bora atoe ili alipe fedha taslimu, hii itaturudisha nyuma badala ya kwenda mbele,” anasema Anitha Mzee mkazi wa Ilala.

Hoja ya Anitha inakuja wakati ambao tayari BoT imeshaagiza watu wanaofanya malipo kwa kutumia kadi wasikatwe tozo yoyote ya malipo, ikiwa ni hatua ya uhamasishaji wa malipo ya kielektroniki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *