
MTWARA: JESHI la Polisi mkoani Mtwara kwa kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vingine vya dola limesema kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka Krismasi na mwaka mpya usalama wa wakazi wa mkoa huo ni shwari.
Akizungumza Desemba 24, 2025 mkoani Mtwara, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara SACP Issa Sulemani amesema jeshi hilo linaendelea kuimarisha usalama katika maeneo yote ya mkoani huo kwa kufanya doria kwenye maeneo yote ya fukwe.
Pia mitaa yote katikati na pambezoni ya mji lengo likiwa ni pamoja na kuhakikisha sikukuu hizo zote za mwisho wa mwaka zinasherehekewa kwa amani na utulivu.
‘’Jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vingine vya dola linaendelea kuimarisha usalama ikiwa ni pamoja na kutoa raarifa kamba usalama wa wakazi wa mkoa wa mtwara kwa ujumla ni shwari’’amesema Sulemani
Aidha jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa dalili zozote za vitendo vya uvunjifu wa amani vitakavyopelekea kutendeka kwa makosa ya kijamii na ya usalama barabarani kwani hatua za haraka zitachukuliwa kwa madereva wote wenye tabia ya kupuuza na kukiuka sheria za usalama barabarani.
Pia limetoa wito kwa wazazi na walezi kutowaacha watoto kwenda katika kumbi na maeneo mengine ya starehe bila ya kuwa na uangalizi ili kuepuka watoto wadogo kupotea, kupata ajali au kufanyiwa vitendo vya ukatili na udharirishaji vinavyoweza kuhatarisha afya na maisha yao.