ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassalla, ametoa wito kwa Watanzania kujenga tabia ya uungwana katika ushindani wa kisiasa ili usiwe chanzo cha kuvunja agano la amani kati yao na Mwenyezi Mungu. Askofu Kassalla ametoa wito huo katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Geita, Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani, mjini Geita, wakati wa maadhimisho ya ibada ya mkesha wa Krismasi.

Amesema ili kuepuka chuki na migogoro ya kisiasa, viongozi na wananchi wanapaswa kujifunza uungwana katika ushindani, maarufu kama fair play kwenye mchezo wa soka, ambapo pamoja na timu kuwa wapinzani, wachezaji husaidiana wanapotokea makosa ili mchezo uendelee kwa amani. SOMA: Polisi Mtwara wajipanga usalama Krismasi

Aidha, alisema Watanzania wanapoadhimisha Sikukuu ya Krismasi wanapaswa kutafakari namna bora ya kuiendea siasa na kuishi kwa misingi ya amani kama ilivyokuwa kwa taifa teule. pia amesisitiza kuwa kila mtu anapaswa kusali, kuishi kwa matendo mema, kukemea vyanzo vya uovu, kusisitiza haki na kutambua thamani ya amani.

Askofu Kassalla aliongeza kuwa Krismasi ni fundisho la mwanzo mpya wa agano la amani, si duniani pekee bali pia mbinguni, na ni mwendelezo wa safari ya ukombozi, hivyo Wakristo wanapaswa kuwa vyombo vya ukombozi wa mwili na nafsi kwa kujenga moyo wa kujitolea kwa wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *