
Dar/Moshi. Wataalamu kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (IAA) wameweka kambi katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, eneo la Barafu, kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha ajali ya helikopta ya kampuni ya uokoaji ya Kilimedair, iliyosababisha vifo vya watu watano.
Ajali hiyo ilitokea jana, Desemba 24, 2025, saa 11:30 jioni, wakati helikopta hiyo ikiwa inatoka kuchukua wagonjwa Mlima Kilimanjaro, kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa.
Maigwa amesema helikopta hiyo ilibeba watu watano, wawili watalii kutoka Jamhuri ya Czech, mmoja muongoza watalii kutoka Tanzania, mmoja daktari Mtanzania, na rubani kutoka Zimbabwe, na wote wamefariki dunia.
Taarifa kuhusu kuwepo kwa wataalamu wanaofanya uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo imetolewa leo, Alhamisi, Desemba 25, 2025, na Kamishna wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Kuji.
Kuji amesema bado chanzo cha ajali hakijabainika na kwamba wataalamu kutoka mamlaka husika, yaani TCAA na TAA, wako katika eneo la tukio kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo na mazingira ya ajali hiyo.
Amewataja waliofariki dunia kuwa ni David Plos (30) na Anna Plosova (30), watalii wa Jamhuri ya Czech, Costantin Mazonde (42), raia wa Zimbabwe, Jimmy Daniel (32), daktari wa kampuni ya uokoaji ya Kilimedair na Innocent Mbaga, muongoza watalii.
“Desemba 24, 2025, saa 11:30 jioni, katika maeneo ya kambi ya kulala wageni ya Barafu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, helikopta ya kampuni ya Kilimedair inayofanya kazi ya uokoaji ilianguka na kusababisha vifo vya watu watano,” amesema.
Amesema watalii hao walianza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro Desemba 20, kupitia njia ya Machame, wakiongozwa na kampuni ya utalii ya Mikaya Tours, na ilikuwa ni safari ya siku sita.
“Ilikuwa ni safari ya kawaida ya utalii ya kupanda mlima, na wakati wa kushuka ndipo hali hiyo ikawakuta. Kabla hawajakamilisha safari yao ya siku sita, jana Desemba 24 walipata ajali na kufariki. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa KCMC,” amesema Kuji.
Kamishna huyo amesema taratibu za kidiplomasia zinafanyika kati ya Serikali na Ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Czech, ili kuona namna ya kukabidhi miili ya watalii waliofariki dunia kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchini kwao.
“Uchunguzi bado unaendelea ili kupata mazingira halisi na chanzo cha ajali, na itifaki zitafanyika kati ya Serikali na Ubalozi wa Jamhuri ya Czech kuona namna ya kushughulikia suala hili. Mara baada ya taratibu kukamilika, tutajulishana,” amesema.