Imepita miaka 58 tangu Rais wa wakati huo wa Somalia, Aden Abdulle Osman, alipokubali kushindwa katika uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa Abdirashid Ali Sharmarke, tukio linalotambuliwa kama makabidhiano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya amani barani Afrika.

Tarehe 25 Disemba, mwelekeo wa kidemokrasia wa Mogadishu unapitia mabadiliko makubwa, kwa kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza ambapo wananchi wameshiriki katika mchakato wa kupiga kura. Tukio hili linakuja wakati muhula wa Rais Hassan Sheikh Mohamud ukikaribia kumalizika Mei 2026, na wabunge wakimaliza muhula wao mwezi mmoja kabla.

Hatua hii ya kihistoria ya ambapo wananchi wanashiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza baada ya karibu miongo sita—inaashiria mwanzo mpya. Tangu 2012 wabunge pekee ndio walikuwa wakipiga kura ya kumchagua rais, hii ni baada ya nchi hiyo kusambaratika kwa zaidi ya miaka 30. 

Hata hivyo, hatua hii imekumbwa na changamoto nyingi, hasa tishio la upinzani kuanzisha “mchakato mbadala wa uchaguzi” huku wakishinikiza mazungumzo mapana kuhusu mwelekeo wa demokrasia ya nchi.

Changamoto zinazotokana na historia ya Somalia

Safari ya Somalia kufikia hatua hii ina mizizi yake katika makabidhiano ya madaraka kwa njia amani ya mwaka 1967 uliofanywa na Rais wa zamani Abdulle Osman. Hata hivyo, yaliyotokea katika kipindi kilichofuata pia yamechangia hali ya sasa ya nchi.

Miaka miwili baada ya kuingia madarakani, Sharmarke aliuawa, jambo lililofungua njia ya mapinduzi ya kijeshi yaliyosimamisha maendeleo ya kidemokrasia kwa miongo kadhaa. Uchaguzi wa chama kimoja uliodhibitiwa wa mwaka 1979 na 1984 ulikuwa ni matukio ya mpito tu, si juhudi za dhati za kurejesha demokrasia.

Ni miaka 13 tu iliyopita ambapo Somalia ilifanya uchaguzi wake wa kwanza wa maana tangu kipindi hicho cha misukosuko. Mchakato huo ulihusisha Bunge lililochaguliwa na wazee wa kimila, na kuashiria mwanzo wa juhudi za kuimarisha mfumo wa uchaguzi usio washirikisha wanachi.

Uchaguzi wa 2016 ulitofautiana na ule wa 2012, ulihusisha wajumbe 14,025 waliowachagua wabunge. Kufikia 2022, idadi ya wajumbe iliongezeka zaidi.

Katika mfumo huu, wabunge 275 pamoja na wajumbe 54 kutoka seneti wamchagua Rais.

Mchakato huu unaongozwa na taratibu kali. Makabila huwasilisha orodha ya wajumbe wao kwa Tume Huru ya Uchaguzi, pamoja na kusajiliwa kwa wazee 135 wenye jukumu la kuwachagua wabunge.

Kila nafasi lazima iwe na wagombea wasiopungua wawili. Uchaguzi wa wabunge hufanyika ndani ya tawala za kikanda, isipokuwa kwa wale wanaowakilisha Somaliland na Banadir, ambao hufanyika Mogadishu.

Baada ya majimbo ya shirikisho na makabila kukamilisha wawakilishi wao, orodha huthibitishwa na kupelekwa mji mkuu. Baada ya uchaguzi kukamilika, Rais mteule humteua Waziri Mkuu ndani ya siku 30, naye hupewa mwezi mmoja kuunda serikali.

Mchakato wa upigaji kura

Mabadiliko ya Somalia kutoka mfumo wa zamani wa upigaji kura yalianza Aprili 2025, wakati Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi na Mipaka (INEBC) ilipoanzisha zoezi la usajili wa wapiga kura Mogadishu. Zaidi ya raia 900,000 walijiandikisha kupiga kura ndani ya muda uliowekwa.

Muundo wa wapiga kura unatoa picha ya kuvutia: takriban 94% ya wapiga kura waliosajiliwa Mogadishu wako chini ya umri wa miaka 44, huku 63% wakiwa wanaume. Idadi ya wapiga kura waliosajiliwa pia ndiyo kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mji mkuu.

Kuongezeka huku kwa ushiriki wa raia kunakwenda sambamba na ushindani mkali wa kisiasa, ambapo vyama 20 vya siasa vimewasimamisha wagombea 1,600 kugombea viti 390.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *