UCHUNGUZI kuhusu ajali ya helikopta ya uokoaji iliyotokea katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA) umeanza kwa lengo la kubaini chanzo cha ajali hiyo iliyotokea juzi na kusababisha vifo vya watu watano.
Hayo yamesemwa na Mhifadhi Mkuu wa Huduma za Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA), Musa Kuji alipokuwa akiwapa taarifa waandishi wa habari kuhusu tukio hilo mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.”Chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana na maofisa wa mamlaka zinazohusika na usafiri wa angani kwa maana ya TCAA na nyingine zinazohusiana na shughuli hizo wako katika eneo la tukio ili kuendelea na uchunguzi,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamishna Kuji, ajali hiyo ilitokea katika eneo la kambi ya barafu lenye urefu wa meta 4,673 kutoka usawa wa bahari ambalo ni sehemu ya Mlima Kilimanjaro. “Ajali hii ilihusisha helikopta ya uokoaji kutoka kwa Kampuni ya KiliMedair na kusababisha vifo vya watu watano akiwemo mwanamke mmoja,” alisema.
Amewataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni rubani wa helikopta hiyo mkazi wa Kata ya Soweto katika Manispaa ya Moshi, Constantin Mazonde (42). “Wengine ni Davis Plos (30) mtalii kutoka Jamhuri ya Czech, Anna Plosova (30) mtalii kutoka Jamhuri ya Czech, Jimmy Daniel (32) daktari kutoka kampuni ya uokoaji ya KiliMedair mkazi wa Kata ya Rau, Manispaa ya Moshi na Innocent Mmbaga mwongoza watalii mkazi wa Jiji la Moshi,” alisema.
Kuji amesema kuwa mawasiliano kati ya mamlaka husika nchini na ubalozi wa Czech nchini tayari yameanza ili utambuzi wa ziada wa wageni waliofariki uweze kukamilika na kukamilisha taratibu nyingine zinazohusiana na msiba wa watu hao ambao waliingia nchini kama watalii. SOMA: ‘Ningekuwepo kwenye ajali iliyomuua Sokoine’
