
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ilijihami kwa njia halali mbele ya uvamizi haramu wa adui, na hatimaye adui akalazimika kuomba kusitisha mapigano bila ya masharti na hivyo, Vita vya Siku 12 vilimalizika kwa heshima na ushindi kwa taifa la Iran.
Katika hotuba yake mbele ya Wanaharakati wa Masuala ya Kiuchumi wa Isfahan, Waziri Abbas Araghchi amesema: Wakati wa vita vya siku 12, tulijilinda kihalali dhidi ya uvamizi haramu wa adui na katika kujibu ombi la adui la kusitisha mapigano au kukomesha vita bila ya masharti, pia tulikubali kusimamisha vita hivyo kwa fakhari si kwa kuburuzwa.”
Amesisitiza kwamba, mwisho wa vita vya siku 12 uliambatana na heshima, ushindi na hadhi maalumu kwa Iran na ushindi huo ulionesha kwamba Muqawama na kusimama imara dhidi ya mashinikizo ya kigeni kunaweza kuleta ushindi wa kujivunia. Wananchi wa Iran wamethibitisha katika historia yote kwamba si watu wa kukubali kudhalilishwa au kuishi kwenye uonevu.
Waziri Araghchi ameongeza kuwa: Iran ni nchi ambayo imekuwa na ustaarabu mkubwa na heshima tukufu katika historia yake ya maelfu ya miaka na haijawahi kuwa chini ya utawala wa kikoloni wa nchi nyingine yoyote.
Amefafanua kwamba, licha ya vikwazo vyote ilivyowekewa Iran kwa makumi ya miaka na licha ya kuwepo madola ya makubwa ya kijeshi katika eneo hili pamoja na propaganda zao zote, lakini tulipata ushindi wa kujivunia katika vita vya siku 12.
Vilevile amesema, adui hivi sasa anajaribu kutumia vibaya matatizo ya kiuchumi kuwafanya wananchi wa Iran waichukie serikali yao, lakini kama ambavyo taifa la Iran limepata ushindi kwenye vita vya siku 12, litapambana pia katika njama za hivi sasa na kuibuka na ushindi wa kujivunia.