
Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea kwenye msikiti ulioko katika Soko la Gamboru, mjini Maiduguri, katika Jimbo la Borno kaskazini-mashariki mwa Nigeria, lililopelekea kuuawa na kujeruhiwa makumi ya Waislamu waliokuwemo msikitini humo.
Shambulio hilo lilitokea Jumanne jioni wakati wa Sala, likilenga mahali pa ibada palipokuwa na waumini wengi na kuongeza orodha ya mashambulio ya kikatili yanayowalenga raia katika eneo hilo linalokumbwa na machafuko.
Mratibu Mkazi wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Nigeria, Mohamed Fall, amesema amehuzunishwa sana na taarifa za watu kupoteza maisha, akilielezea tukio hilo kuwa ni “shambulio la kinyama dhidi ya raia wasio na hatia.”
“Shambulio hilo, lililotokea wakati wa Sala ya Magharibi, lilisababisha kupotea kwa maisha na kuwaacha wengi wakiwa wamejeruhiwa,” amesema Fall katika taarifa iliyotolewa mjini Abuja.
Kwa mujibu wa duru za habari Waislamu watano wameuawa na wengine zaidi ya 30 wamejeruhiwa katika shambulio hilo.
“Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa nchini Nigeria, ninatoa rambirambi zangu za dhati kwa familia za waliopoteza maisha, na kwa serikali na wananchi wa Jimbo la Borno,” ameeleza afisa huyo wa UN huku akiwatakia majeruhi “afuweni ya haraka.”
Aidha, Fall amejiunga na Gavana wa Jimbo la Borno, Profesa Babagana Umara Zulum, kulaani vikali shambulio hilo, akisisitiza kuwa maeneo ya ibada hayapasi kamwe kulengwa.
Mratibu huyo Mkazi wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Nigeria amesisitizia pia kuongezwa umakini na kuimarishwa hatua za usalama, hususan katika kipindi hiki cha sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.
“Huu ni wakati ambao jamii zinapaswa kukusanyika kwa amani, si kwa hofu,” ameongezea kusema afisa huyo wa UN…/