Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF nchini Sudan vimetangaza kwamba vimezidisha mashambulizi na kuchukua udhibiti wa maeneo ya Abu Qamra na Ombro katika jimbo la Darfur Kaskazini, huko magharibi mwa Sudan.

Mwandishi wa televisheni ya Al-Alam ameripoti kutoka nchini Sudan akizinukuu duru za ndani ya nchi hiyo zikithibitisha kwamba Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vimevamia eneo la Abu Qamra vikiwa na magari mengi ya kivita na kusambaza video kwenye mitandao ya kijamii zinazowaonesha wakisonga mbele kwenye eneo hilo.

Vyombo vya ndani ya Sudan vimetangaza kuwa mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu wengi na majeruhi kutoka pande zote mbili za RSF na SAF. Huku Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vikijaribu kuchukua udhibiti wa jimbo lote la Darfur Kaskazini, jeshi la Sudan SAF na vikosi linavyoshirikiana navyo bado vinadhibiti baadhi ya maeneo ya jimbo hilo.

Harakati ya Ukombozi wa Sudan inayoongozwa na Abdul Wahid Nur pia inadhibiti baadhi ya maeneo ya jimbo la Darfur Kaskazini. Hayo yamekuja siku chache baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kusisitizia umuhimu wa kukomeshwa mapigano nchini Sudan na kuonya kuhusu athari mbaya za kuendelea mapigano nchini humo.

Mohamed Khaled al-Khiari, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya Kisiasa na Amani, amesema: Matukio ya nchini Sudan yanaonyesha utambulisho unaozidi kuwa tata wa mzozo huu na kuchukua wigo mpana kikanda, na ikiwa hakutachukuliwa hatua za kuupatia ufumbuzi basi kuna uwezekano hatari yake ikayakumba pia majirani wa Sudan.”

Onyo hili linakuja wakati Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu amekuwa akionya kwa miezi kadhaa sasa kuhusu hatari za kuongezeka kwa uhasama katika maeneo mbalimbali kama vile Kordofan na kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuzuia kukaririwa uhalifu uliorekodiwa katika Darfur Kaskazini, hasa El-Fasher.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *