
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea na mchakato wa kutekeleza mradi wa Bomba la Gesi kutoka Kinyerezi kwenda Chalinze utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni 2.3.
Akizungumza kwenye kikao na uongozi wa Mkoa wa Pwani kujadili namna ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Mussa Makame alisema mradi huo kwa sasa umekamilisha hatua ya upembuzi yakinifu. Makame alisema bomba hilo la gesi litapita sambamba na njia za umeme chini ya usimamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alisema kuwa mradi huo ni miongoni mwa jitihada za serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuufanya Mkoa wa Pwani kuwa mkoa wa kimkakati kiuchumi. SOMA: Ujenzi bomba la gesi kuanza Mtwara
Kunenge amesema utekelezaji wa mradi huo utachochea uwekezaji hususani katika sekta ya viwanda hali itakayoongeza uzalishaji kuimarisha ajira na kukuza mapato ya mkoa. Amesema umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Mkoa wa Pwani na TPDC ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
Akiwasilisha taarifa ya kina ya mradi, Angelindile Marandu amesema kuwa mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya Gulf Interstate Engineering kwa kushirikiana na Paulsam Geo-Engineering Co. Ltd. Marandu amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15 tangu tarehe ya kusainiwa kwa mkataba wa mradi.