Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imetoa simulizi yake ya pili kuhusiana na Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa dhidi ya Israel iliyoendeshwa kwa mafanikio Oktoba 7, 2023, ikisisitiza kwamba, Muqawama wa wananchi wa Palestina dhidi ya utawala katili wa Kizayuni hauwezi kusambaratishwa.

Katika simulizi yake mpya yenye kichwa cha maneno “Simulizi Yetu… Kimbunga cha al Aqsa: Miaka Miwili ya Muqawama na Nia Thabiti ya Ukombozi,” Hamas imesema kuwa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Wapalestina walikuwa ni “kitovu cha uthabiti na ustahimilivu” mbele ya moja ya vita vya kikatili zaidi na vya uangamizaji mkubwa zaidi vilivyolenga kuvunja imani yao na kuwalazimisha kujisalimisha kidhalili mbele ya adui, na wameibuka na ushindi wa kifakhari kwenye mtihani huo mzito.

Katika kipindi cha miaka miwili ya mauaji ya kimbari, Israel ilikuwa inatangaza kwamba lengo lakeni kuangamiza kizazi cha Wapalestina kupitia kuwahamisha kutoka kwenye Ukanda wa Ghaza na kusambaratisha Muqawama wao, lakini wameshindwa vibaya.

Katika hati yake ya kurasa 42, HAMAS imesema: “Baada ya miaka miwili ya mauaji ya kimbari na kusimama thabiti taifa la Palestina, simulizi yetu leo hii inatangaza wazi kwamba, watu ambao hawawezi kufutwa, Muqawama ambao hauwezi kushindwa na kumbukumbu ambayo haiwezi kusahaulika ni ya matukio ya miaka miwili yaliyokuja baada ya operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa.”

Israel ilianzisha mashambulio ya kikatili dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba, 2023, baada ya Hamas kuendesha operesheni yake ya Kimbunga cha al Aqsa ya kulipiza kisasi jinai za Israel. Licha ya mashambulizi ya kinyama ya Israel kuua kwa umati Wapalestina wasiopungua 70,942, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine 171,195 lakini ilishindwa kufikia malengo yake iliyoyatangaza; na jeraha la pigo la Kimbunga cha al Aqsa haliwezi kupona hata siku moja katika mwili uliojaa nuhsi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *