
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema amefanya mazungumzo yenye tija na mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff na mkwe wake Jared Kushner jinsi ya kuvimaliza vita na Urusi.
Zelenskyy ameyasema hayo katika chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram akiongeza kwamba wameweka wazi mawazo na mbinu mpya zenye lengo la kusaidia namna ya kupatikana kwa amani na kufikia makubaliano.
Katika siku hizi za hivi karibuni, juhudi za Marekani ambayo ni mpatanishi wa mzozo huo zimekuwa zikiongozwa na wajumbe hao wawili ingawa matokeo ya jitihada hizo bado ni ya pole mnoo.
Urusi kupitia msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Maria Zakharova imekiri kwamba mazungumzo hayo ya kumaliza vita hivyo vyenye karibu miaka minne na yanayoongozwa na Marekani yamepiga hatua chache.