
Wakazi wa Mogadishu Kuu wamepiga kura mnamo Desemba 25 katika uchaguzi wao wa kwanza wa serikali za mitaa kwa kupiga kura moja kwa moja tangu miaka 56 iliyopita. Uchaguzi huo ulihusu eneo la Banadir, ambapo mji mkuu wa Mogadishu upo, kusini mashariki mwa nchi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu jijini Nairobi, Albane Thirouard
Nchini Somalia, katika eneo la mji mkuu, foleni ndefu zilishuhudiwa nje ya vituo vya kupigia kura mapema asubuhi ya Desemba 25. Wapiga kura waliliambia shirika la habari la AFP kwamba walifurahi kutimiza wajibu wao wa kiraia. “Tumefungua ukurasa mpya katika historia yetu,” Rais Hassan Sheikh Mohamud alitangaza.
Isipokuwa uchaguzi uliofanyika katika eneo linalojitawala la Puntland na eneo lililojitenga la Somaliland, Somalia ilifanya uchaguzi wa moja kwa moja mara ya mwisho mwaka wa 1969, muda mfupi kabla ya dikteta wa zamani Siad Barre kuingia madarakani. Uchaguzi wa serikali za mitaa wa Alhamisi ulikuwa kipimo muhimu kwa serikali ya shirikisho. Umefayika kwa amani, licha ya ukosoaji kutoka kwa upinzani.
Vituo vya kupigia kura vilifungwa salama katika eneo la Banadir, ambalo linajumuisha mji mkuu Mogadishu, kulingana na tume ya uchaguzi. Uwepo mkubwa wa vikosi vya usalama na jeshi ulikuwepo huku nchi ikipambana na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Al-Shabab. Maafisa wa usalama 10,000 walitumwa, usafiri ulipunguzwa katika mji mkuu, na uwanja wa ndege ulifungwa.
Kwa Hassan Sheikh Mohamud, lengo lilikuwa kuonyesha uwezo wa Somalia wa kufanya uchaguzi wa moja kwa moja kabla ya uchaguzi wa wabunge na ule wa urais uliopangwa kufanyika mwaka wa 2026. Ilikuwa chini ya utawala wake ambapo mpito wa kupiga kura moja kwa moja ulipitishwa mwaka jana. Hata hivyo, mageuzi hayo yamekabiliwa na ukosoaji mkubwa. Vyama vikuu vya upinzani vilisusia uchaguzi wa serikali za mitaa na tayari vimepinga matokeo, vikitaja wasiwasi kuhusu uaminifu wa uchaguzi.
Upinzani unalaani mageuzi ya kupiga kura moja kwa moja kama “ya upande mmoja,” unamshutumu rais kwa kutaka kuahirisha uchaguzi wa mwaka 2026, na unatishia kuandaa mchakato sambamba ikiwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa. Hassan Sheikh Mohamud alisema yuko tayari kwa mazungumzo, alipoondoka kituo cha kupigia kura.