
Kamanda wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria (SDF), Mazloum Abdi amesema katika taarifa kwamba suluhisho pekee la matatizo ya Syria ni kuachana na mfumo wa utawala uliopita na kuelekea kwenye serikali ya shirikisho.
Abdi ameongeza kuwa: Ugatuzi wa kisiasa unaojumuisha mgawanyo wa madaraka kati ya serikali kuu na majimbo ndio suluhisho pekee la matatizo na lenye kutoa hakikisho kwa mustakabali wa Syria.
Kiongozi huyo wa Wakurdi wa Syria amesema kuna uwezekano mdogo mno wa kufeli mazungumzo kati ya SDF na serikali ya mpito na akabainisha kuwa: sinario hiyo ni dhaifu na kwamba kufeli kwa mazungumzo kutakuwa na madhara kwa taifa zima la Syria.
Abdi ameeleza kwamba, mazungumzo ya moja kwa moja na yasiyo ya moja kwa moja na serikali ya Damascus hayajasimama licha ya kuwepo ukiukwaji; na makubaliano yaliyosainiwa na kiongozi wa serikali ya mpito hayana kikomo maalumu cha muda wa utekelezaji.
Aidha, amesisitiza kuwa, utajiri na rasilimali za nchi ni za wananchi wote na lazima zigawanywe kwa usawa miongoni mwao.
Kamanda huyo wa SDF ametoa indhari pia kuhusu ufuatiliaji unaodaiwa kufanywa na serikali ya Damascus kwa wafanyakazi wa serikali Wakurdi inayojiendeshea mambo yake, akiielezea hatua hiyo kuwa ni ya kuchochea mvutano.
Inafaa kuashiria kuwa, wakati tarehe ya mwisho iliyowekwa kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya mpito ya Syria na Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria (SDF) inakaribia, matukio ya kisiasa na ya ugani nchini Syria yameingia kwenye awamu muhimu na hasasi; awamu ambayo, pamoja na mashinikizo yanayoongezeka kutoka Damascus na serikali ya Uturuki, inaashiria kuongezeka huko mvutano kaskazini mwa nchi, na kuuweka mustakabali wa makubaliano hayo katika wingu la hatihati…/