Wizara ya Kilimo ya Palestina imetangaza kuwa, ndani ya muda wa wiki moja, uvamizi uliofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel na walowezi haramu umeharibu zaidi ya mizeituni 8,000 katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kusababisha hasara ya karibu dola milioni saba.

Katika ripoti yake ya kila wiki, wizara hiyo ilieleza jana Alkhamisi kwamba ardhi za Palestina zimeshuhudia “kuongezeka kwa hatari na kwa kasi” mashambulizi ya jeshi la Israel na walowezi haramu, yakilenga moja kwa moja sekta ya kilimo na vyanzo vya usalama wa chakula.

Wizara hiyo imesema, mashambulizi hayo, yaliyotokea wakati wa wiki ya tatu ya mwezi huu wa Desemba, yalikuwa sehemu ya sera ya kimfumo inayolenga “kunyakua ardhi ya Palestina na kuwaondoa wakazi wake wa asili.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashambulizi ya Israel yalijikita katika Ukingo wa Magharibi wa kaskazini na kati, ambapo jeshi la kizayuni liling’oa miti ya mizeituni 5,000 katika mji wa Silat al-Harithiya magharibi mwa Jenin kaskazini, na miti mingine 3,000 ya mizeituni huko Turmus Ayya, mashariki mwa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa kati.

Wizara ya kilimo ya Palestina imerekodi pia uharibifu holela wa ung’oaji miti ya mizeituni 156 Mashariki mwa Baitul Muqaddas, miti ya mitini 100 huko Tulkarem, miti ya mizeituni 13 mashariki mwa Qalqilya, na miti ya mizeituni 19, ikiwa ni pamoja na miti 10 ya kale, huko Salfit na Bethlehem.

Ripoti hiyo imesajili pia uharibifu wa miundombinu ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kubomolewa visima 13 vya maji na vitalu vya kilimo, uharibifu wa mitandao ya umwagiliaji na wizi wa pampu za maji, uharibifu wa mizinga 82 ya nyuki, na kuilisha sumu mifugo ya kondoo katika maeneo mbalimbali.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika uamuzi wa kihistoria uliotolewa Julai mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ilitangaza kuwa, uvamizi uliofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel katika eneo la Palestina uko kinyume cha sheria na ukataka kuondolewa vitongoji vyote katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baitul Muqaddas Mashariki…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *