Dar es Salaam. Zuberi Foba na Prince Dube, ni kati ya nyota 25 kutoka Ligi Kuu Bara wanaoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 zinazoendelea nchini Morocco, huku namba zao zikiwabeba baada ya kumalizika kwa raundi ya kwanza hatua ya makundi.

Kuanza kwao vizuri kutokana na takwimu zilizotolewa na Sofascore baada ya kumalizika kwa raundi hiyo, inabaki kuwa mtihani kwao kuelekea mechi za pili ambapo Dube leo Ijumaa atakuwa uwanjani pale Zimbabwe itakapoikabili Angola. Timu hizo zote zilipoteza mechi ya kwanza kwa mabao 2-1.

Kesho Jumamosi inakuwa zamu ya Foba kulinda milingoti mitatu ya Taifa Stars itakapopambana na Uganda. Mechi ya kwanza Stars ilifungwa 2-1 na Nigeria, Uganda ikachapwa 3-1 na Tunisia.

Kupoteza kwa Zimbabwe na Taifa Stars, kunawapa nafasi nyingine Dube na Foba kuzibeba timu hizo kupata ushindi wa kwanza na kuchonga njia ya kufuzu hatua ya 16 bora.

Golkipa wa Azam FC na Taifa Stars, Zuberi Foba.

Fainali za AFCON 2025 zilizoanza Desemba 21, mwaka huu nchini Morocco, Ligi Kuu Bara inawakilishwa na nyota hao 25 kutoka klabu tano pekee ambazo ni Simba inao nane, Yanga wapo sita, Azam na Singida Black Stars kila moja ina watano na Pamba Jiji mmoja.

Mastaa wa Simba waliopo AFCON ni Steven Mukwala (Uganda), Yakoub Suleiman (Tanzania), Shomari Kapombe (Tanzania), Wilson Nangu (Tanzania), Yusuph Kagoma (Tanzania), Morice Abraham (Tanzania), Kibu Dennis (Tanzania) na Seleman Mwalimu (Tanzania).

Kwa upande wa Yanga kuna Djigui Diarra (Mali), Prince Dube (Zimbabwe), Bakari Mwamnyeto (Tanzania), Mohamed Hussein (Tanzania), Ibrahim Hamad (Tanzania) na Dickson Job (Tanzania).

Singida Black Stars inawakilishwa na Amas Obasogie (Nigeria), Khalid Aucho (Uganda), Hussein Masalanga (Tanzania), Nickson Kibabage (Tanzania) na Habibu Idd (Tanzania).

Azam wapo Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Iddi Suleiman na Feisal Salum ambao wote wanaunda kikosi cha Tanzania, huku Pamba Jiji akiwepo Kelvin Nashon (Tanzania).

Wakati juzi Jumatano raundi ya kwanza hatua ya makundi ikifikia tamati, nyota 11 kutoka Ligi Kuu Bara ndiyo walipata nafasi ya kucheza kati ya 25 waliopo huko, huku ikishuhudiwa Dube pekee akianza na mguu mzuri wa kutikisa nyavu.

Dube katika mechi ya kwanza dhidi ya Misri, alicheza kwa dakika 72, akafunga bao pekee walipopoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Misri.

Mshambuliaji wa Yanga na timu ya Taifa, Zimbabwe akishangilia baada ya kufunga bao dhidi ya Misri.

Mshambuliaji huyo aliyemaliza na mabao 13 msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara akiichezea Yanga, dhidi ya Misri katika dakika 72 alizocheza kabla ya kumpisha Tawanda Chirewa, alifanya vitu vichache lakini vyenye maana kubwa na kupewa alama 7.4 na mtandao wa Sofascore kutokana na kiwango alichoonyesha.

Takwimu hizo zinamuonyesha Dube alikuwa na wastani wa asilimia 67 wa pasi za uhakika alizopiga, huku mpira mmoja mrefu aliopiga ukimfikia mlengwa kwa usahihi.

Ukimuweka kando Dube ambaye bao alilofunga ndilo limempa nafasi ya kuonekana kuwa na takwimu bora zaidi ya mastaa wengine wa Ligi Kuu Bara waliopo AFCON, pia kipa wa Azam na Taifa Stars, Zuber Foba amewashangaza wengi.

Foba aliyedaka mechi yake ya kwanza AFCON kwa dakika zote tisini na kuruhusu mabao mawili katika kichapo cha 2-1 dhidi ya Nigeria, amepewa alama 8.3, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kwa wachezaji wote kwenye mechi hiyo ya kundi C.

Hali hiyo imemfanya Foba aliyefanya sevu nane kuwa na alama nyingi zaidi ya mchezaji bora wa mechi hiyo na mfungaji wa bao la kwanza Semi Ajayi aliyepewa 8.0 na Alex Iwobi aliyetoa asisti zote mbili akipata 8.2.

Nyota anayefuatia kwa kuonekana kucheza kwa kiwango kizuri ni Mwamnyeto aliyepewa alama 7.3 kutokana na kucheza dakika zote tisini dhidi ya Nigeria.

Mwamnyeto katika dakika hizo, alishiriki mara 13 kuzuia mashambulizi, huku takolini moja pekee aliyofanya ilikuwa ya usahihi kwa asilimia mia moja akiwa hajapitwa na mpinzani muda wote wa mechi.

Kwa upande wa kuondoa hatari, alifanya mara kumi, huku akizuia mashuti mawili kuelekea langoni kwao sambamba na kupokonya mpira mara mbili. Pia Mwamnyeto aliokoa hatari moja katika mstari wa goli.

Katika kuwania mipira ya juu alifanikiwa mara zote mbili alizofanya, pia akafanikiwa kuwania mipira mitatu ya chini kwa asilimia mia moja.

Job licha ya kutokea benchi akicheza kwa dakika 11 alipochukua nafasi ya Tarryn Allarakhia, amepewa alama 7.2 kutokana na utulivu na majukumu aliyofanya ndani ya uwanja.

Job alishiriki mara tatu kuzuia mashambulizi ya Nigeria, huku akishinda takolini moja kati ya mbili alizofanya na kuokoa hatari moja sambamba na kupokonya mpira mara moja.

Kwa upande wa kuwania mipira ya chini, alifanikiwa mara zote mbili alizofanya, huku akiwa hajapitwa na mpinzani.

Kiungo wa Singida Black Stars, Khalid Aucho, aliiongoza Uganda dakika zote tisini na kupoteza mechi kwa mabao 3-1 dhidi ya Tunisia, lakini kile alichokifanya, amepewa alama 7.0.

Aucho katika nafasi yake ya kiungo wa kati, alipiga pasi 51, kati ya hizo 44 zilikuwa sahihi, huku mipira mitatu mirefu aliyopiga, mmoja pekee ndiyo ulifika kwa usahihi.

Nafasi ya sita inashikwa na Shomari Kapombe aliyepata alama 6.9 kutokana na kushiriki mara saba katika kuzuia mashambulizi, lakini takolini nne alizofanya, hakuna hata moja aliyofanikiwa japo alifanya kwa usahihi kuokoa hatari mbili.

Kapombe ambaye ni beki wa kulia wa Taifa Stars na klabu ya Simba, alifanikiwa kupokonya mpira mara moja na kushinda mipira ya chini mara sita kati ya tisa aliyopambania, huku akishinda mpira mmoja tu wa juu kati ya minne. Alipitwa mara tatu na wapinzani.

Mshambuliaji wa Simba na Uganda, Steven Mukwala, amepewa alama 6.5 kutokana na kucheza dakika 71 dhidi ya Tunisia, akampisha James Bogere.

Hakufunga bao wala kutoa pasi ya bao, lakini alipiga mashuti mawili pekee moja likizuiwa na kumfanya kutokuwa na shuti lililolenga lango.

Beki wa Taifa Stars na Yanga, Ibrahim Hamad anakuwa mchezaji wa nane katika listi hii akipewa alama 6.4 kutokana na kucheza dakika tisini dhidi ya Nigeria akishiriki mara 16 kuzuia mashambulizi.

Takolini moja aliyopiga ilikuwa ya usahihi, huku akiokoa hatari 13 na kuzuia shuti moja lisielekee golini.

Katika kuwania mipira ya chini, alifanikiwa mara nne kati ya nane, huku akishinda mipira ya juu mara moja kati ya tano. Alicheza faulo mbili na kupitwa mara mbili na wapinzani.

Beki mwingine wa Yanga, Mohamed Hussein amepewa alama 6.3 kutokana na dakika tisini alizocheza Taifa Stars dhidi ya Nigeria akishiriki mara tano kuzuia mashambulizi, huku akifanya takolini mbili zote kwa usahihi na kuokoa hatari mbili.

Beki huyo aliyetua Yanga msimu huu, alipokonya mpira mara tisa, akishinda mipira mitatu ya chini kati ya minane aliyowania, huku akishindwa kuwania mipira ya juu kati ya mara moja aliyojaribu kufanya hivyo. Pia alipitwa na wapinzani mara nne.

Kipa namba moja wa Yanga na Mali, Djigui Diarra alikuwa langoni wakati wakitoka sare ya 1-1 dhidi ya Zambia. Bao aliloruhusu dakika ya 90+2, lilimtibulia kwani alishindwa kulinda clean sheet zikibaki sekunde chache kabla ya mechi kumalizika.

Dakika tisini alizocheza katika mechi hiyo, amepewa alama 6.0, kutokana na kulindwa vizuri na mabeki wake, alifanya sevu moja pekee.

Nyota mwingine aliyepata nafasi ya kucheza AFCON 2025 kutokea Ligi Kuu Bara hadi sasa ni Kibu Denis wa Simba ambaye aliingia dakika za nyongeza baada ya kutimia 90 akichukua nafasi ya Charles M’mombwa wakati Taifa Stars ikifungwa 2-1 na Nigeria.

Kibu kwa muda alioingia, alicheza dakika moja pekee ambayo haikumpa nafasi nzuri ya kuonyesha kile alichonacho.

Akizungumzia nafasi aliyopata katika michuano ya AFCON 2025, Foba alisema: “Baada ya kupewa nafasi nilijiamini nikifahamu kwamba nakwenda kucheza mchezo mgumu dhidi ya wachezaji wakubwa.

“Nilijipa moyo mwenyewe, pia wachezaji wenzangu walinipa moyo kwamba ninaweza ndio maana nimekuwa hapa, nadhani hiyo ndio imefanya mpaka imekuwa hivi.

“Kilichobaki tuombeane katika michezo ijayo tulisogeze taifa pale tunapotaka kulisogeza. Kwa mimi naamini tunaweza kuvuka hatua ya makundi,” alisema Foba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *