Mwimbaji wa Bongo Fleva, Jux ambaye pia ni mkali wa mitindo ya mavazi, amefanikisha mengi kwa huu uliobakiza siku chache kumalizika, huku mengine yakiweka rekodi ya kipekee kwa upande wake.
Jux anayefanya vizuri na wimbo wake mpya, Majo (2025), ameupiga mwingi kuanzia maisha yake binafsi hadi katika muziki uliomtambulisha kwa wengi. Na haya ni baadhi tu.
1. Ndoa na mtoto
Upande wa familia, kwa Jux mwaka huu amepata neema kubwa kwani amefunga ndoa kwa mara ya kwanza, kisha kujaliwa mtoto wake wa kwanza na kumpa jina la Rakeem Mkambara.
Februari ndipo Jux alifunga ndoa na mpenzi wake kutokea Nigeria, Priscilla anayejulikana zaidi mtandaoni kama Priscy ambaye waliweka wazi uhusiano wao mnamo Julai 2024.
Kufikia Aprili, wakafanya sherehe mbili ikiwemo ya kimila huko Nigeria, kisha Mei wakafanya nyingine Dar es Salaam na kukutanisha mastaa kibao kutokea Bongo na hata Nollywood.
Julai 24, katika Instagram wakatangaza wanatarajia kupata mtoto, posti hiyo walioshirikiana ndio posti yao iliyofanya vizuri zaidi Insta kwa muda wote ikiwa imepata likes milioni 1.1, na kupokea maoni 91,600.
Walitangaza kuzaliwa kwa mtoto wao mwishoni mwa Agosti, ikiwa ni takribani miezi miwili tangu Jux atoe wimbo, Thank You (2025) kwa ajili yake.
Oktoba 2 wakamfanyia sherehe ya kutimiza siku 40 nyumbani kwao Mbezi Beach, Dar es Salaam. Kwa sasa Jux na Priscilla hawatambuliki tu kama ‘kapo’ yenye ushawishi, bali kama familia pia.
2. EP ya kwanza
Mnamo Mei, Jux aliachia Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, A Day To Remember (2025) yenye nyimbo saba ila tatu kati ya hizo zilikuwa zishatoka awali ambazo ni Si Mimi, God Design na Ex wa nani.
EP hii ni kwa ajili ya kumbukumbu ya ndoa yake na mkewe Priscilla na moja ya picha za harusi yao ndiyo imetumika katika cover la EP hiyo yenye mahadhi ya Bongo Fleva na Afrobeats.
Vilevile hii ni zawadi maalum kwa mashabiki wake waliokuwa na kiu ya kusikia tena sauti yake laini na simulizi za kimapenzi anazozijua vizuri.
Huu ni mkusanyiko wa nyimbo zinazochangamsha na zilizobeba hisi kali, kwa ujumla zinaonesha ukuaji wa Jux kama msanii na msimulizi mzuri wa hadithi za mapenzi kupitia muziki.
Utakumbuka Jux, mwanachama wa zamani wa kundi Wakacha, amekuja na EP baada ya kutoa albamu zake mbili, The Love Album (2019) na King of Hearts (2022) chini ya chapa yake maarufu ya African Boy.
3. Tuzo za kimataifa
Tangu alipofanya vizuri na wimbo wake, Ololufe Mi (2024) akimshirikisha Diamond Platnumz, kisha God Design (2025) akiwa na rapa Phyno kutokea Nigeria, Jux ameshinda tuzo kadhaa za kimataifa.
Februari 2025, Jux alishinda tuzo za Trace zilizofanyika Zanzibar akiibuka kidedea katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Tanzania, huku Nandy akishinda kama Msanii Bora wa Kike.
Hata hivyo, wasanii hao walikuja kukabidhiwa tuzo hizo Machi katika hafla maalumu iliyofanyika Dar es Salaam baada ya ile ya Zanzibar kukumbana na changamoto ya hali ya hewa.
Aprili 2025, huko Lagos, Nigeria, Jux akashinda tuzo ya Headies kama Msanii Bora Afrika Mashariki 2025 akiwabwaga Bien (Kenya), Diamond Platnumz (Tanzanaia), Bruce Melodie (Rwanda) na Azawi (Uganda).
Kufikia Novemba 2025, Jux kupitia wimbo wake ‘Ololufe Mi’ akashinda tuzo ya Jayli zilizofanyika jijini Abidjan, Ivory Coast, huku napo alishinda kama Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki 2025.
Jux aliwabwaga Marioo (Nairobi), Diamond (Nitafanyaje), Willy Paul & Bahati (Keki), Abigail Chams (Me Too), Harmonize (Furaha), Zuchu (Antena), Joel Lwaga (Olodumare), Mbosso (Pawa) na Barnaba (Salama).