MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita ametoa ahadi kwa watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu kuwanunulia sare za shule na kuwalipia bima ya afya ili waweze kupata matibabu.
Mhita ametoa Ahadi hiyo wakati wa kushiriki chakula cha pamoja na watoto hao kusherehekea sikukuu ya krisimasi akiwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wa dini.

Mkuu huyo wa mkoa ameomba apate orodha ya idadi ya watoto wote yatima na wanaoishi katika mazingira Mmgumu kutoka kwa walezi wa vituo kwa kushirikiana pia na Maafisa Ustawi wa Jamii ili kufanikisha suala hilo.
Amesema inapofika siku za msimu wa sikukuu kila mtu huwa anamkimbilia mtu ambaye anamfahamu kwa ajili ya kumshika mkono kupata chochote lakini watoto hao hawana wa kuwakimbilia hivyo ameamua kubeba jukumu hilo la kufurahi nao.

“Najiuliza watoto hawa Malaika, ambao hawana wazazi na wengine kuachwa na kuishi mazingira magumu huwa wanamkimbilia nani katika sherehe hizi za sikukuu na mahitaji ya shule ili wafurahi kama watoto wengine,”amesema Mhita.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi amempongeza mkuu huyo wa mkoa wa aliouonyesha kwa watoto hao kwa matendo ya huruma.
“Natoa wito kwa wazazi kuwalea watoto wao kwa mujibu wa sheria na siyo kuwaacha wakiishi mazingira magumu huku mitaani na kuhakikisha ulinzi na usalama wao,”amesema Magomi.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo amesema upendo ni jambo la kiroho kwa kuthamini watoto hao na kwamba Manispaa hiyo itaendelea kusaidia watoto hao kupitia Maafisa Ustawi wa jamii.
Mwakilishi wavVituo vya kulea watoto hao Zainab Ramadhani kutoka kituo cha Taqwa kilichopo Bulugalila kata ya Kizumbi ameshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kujumuika na watoto hao na ahadi aliyoitoa.