
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesisitiza kuwa, uwezo wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran utaendelea kuwepo na kwamba: “Maadui watakumbana na usiku wa giza kama wanataka kuidhuru Jamhuri ya Kiislamu.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya jiji la Tehran amesisitiza pia kuwa Iran ni ile ile yenye nguvu iliyoigeuza miji ya Tel Aviv na Haifa kuwa mahame na amesisitiza kwa kusema: “Ninawaomba wakuu wa jeshi wasitume ujumbe dhaifu.” Amesema, nara ya “Iran yenye nguvu” ni nara Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. “Hii ni kwa sababu shaari ya kuwa na nguvu ina mizizi yake katika Qur’ani Tukufu, ambayo inawakhutubu Waislamu kwa kusema, “Na waandalie nguvu yoyote uwezayo.” Yaani uwe na nguvu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijeshi n.k.
“Madola ya watu waoga ya kimataifa yanafanya kila yawezalo kuhakikisha kuwa Iran inaachana na nguvu zake za makombora. Hivi sasa ambapo Iran ina uwezo mkubwa sana wa makombora na zaidi ya hayo, tunakwambieni nyinyi na maadui wote wa Iran kwamba mkithubutu kuudhuru mfumo huu, siku yenu itageuka kuwa usiku wa giza totoro,” amesema Ayatullah Khatami katika khutba za Sala ya Ijumaa ya leo ya hapa mjini Tehran.
Imam wa Sala ya Ijumaa ya jiji la Tehran ameeleza kuwa, adui anauogopa Uislamu na kuongeza kuwa: “Adui hataki Iran iwe taifa la Kiislamu na anataka kuipindua Jamhuri ya Kiislamu, na njia pekee ya kukabiliana na njama hizo za adui ni ile aliyosema Kiongozi Muadhamu, yaani tuwe na Iran yenye nguvu; na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Iran yenye nguvu itawaangamiza maadui.
Katika sehemu nyingine ya khutba za Sala ya Ijumaa ya leo ya hapa Tehran, Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami ametoa mkono wa kheri kwa Wakristo wa hapa nchini na ulimwenguni kote kwa kusherehekea X-Mass na katika kuukaribisha Mwaka Mpya wa Miladia wa (2026) na kusema: “Ninawaomba Wakristo duniani kote wawe pambo la Nabii Isa AS. Hii ni kwa sababu Nabii Isa alikuwa kitovu cha upendo kwa waja wa Mwenyezi Mungu.