
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametahadrharishakatika ripoti yao wiki hii kwamba kundi lenye misimamo mikali la al Shabab lingali ni tishio kubwa hivi sasa kwa amani na uthabiti huko Somalia na katika eneo zima pa Pembe ya Afrika ikiwa ni pamoja na katika nchi jirani ya Kenya.
Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa wanagambo wa al Shabab bado wana uwezo wa kutekeleza mahambulizi makubwa licha ya juhudi zinazoendelea za kijeshi za vikosi vya Somalia na kimataifa vya kukokemesha hujuma za kundi hilo.
Kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida si tu linatekeleza mashambulizi makubwa lakini pia limeendelea kudumisha mtandao wa wa unyang’anyi, wa kusajili kwa lazima wapiganaji kujiunga na kundi hilo na kuendelesha propaganda athirifu.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameashiria jaribio la mauaji ya Rais wa Somalia mnamo Machi 18 mwaka huu huko Mogadishu mji mkuu wa Somalia na kusisitiza kuhusu hatari ya kundi hilo huko Mogadishu.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumanne wiki hii lilipiga kura na kurefusha muda wa kuhudumu kikosi cha askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AU) huko Somalia hadi Disemba 31 mwaka kesho. Kikosi hicho kinachojumuisha wafanyakazi 11,826 kina jukumu kuu la kulinda amani na kudumisha utulivu huku kukiwa na vitisho vinavyoendelea kutoka kwa al-Shabab.
Kundi la al Shabab pia limekuwa likijipenyeza katika nchi jirani ya Kenya kwka kufanya mashambulizi mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kutega mabomu na mada za milipuko, kuteka nyara watu khususan katika kaunti za Kenya zinazopakana na Somalia. Ripoti hiyo imefichua kuwa al-Shabab mwaka huu kwa wastani imefanya mashambulizi sita huko Kenya.
Timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa pia imeeleza wasiwasi wao kuhusu kuimarika kundi la kigaidi la Daesh huko Somalia na kueleza kuwa ingawa uwepo huo ni wa kiwango cha chini ikilinganishwa na al-Shabab, lakini kuendelea kujiimarisha kundi hilo nchini Somalia ni tishio kubwa la usalama wa eneo la Pembe ya Afrika.