
Israel Katz Waziri wa Vita wa Israel amesisitiza kuwa Tel Aviv “kamwe haitaondoka ” Gaza, na kwamba watajenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa ukanda huo, hatua ambayo ni kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano.
Katz amesisitiza kuwa Israe haitaondoka Gaza na kwamba itaanzisha eneo pana kwa jina la “Buffer Zone” katika Ukanda wa Gaza. Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni amebainisha haya huku Israel ikitakiwa kuondoka kikamilifu huko Gaza kwa mujibu wa mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kusimamisha vita wenye vipengee 20.
Jana Alhamisi Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni alikadhibisha taarifa kwamba amejiuzulu na kusema Israel Israel itachukua hatua huko Gaza sawa na zile alizozitaja kuwa sera zinazotekelezwa na utawala huo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Israel ilivamia na kulikalia kwa mabavu eneo la Ukingo wa Magharibi tangu mwaka 1967 na ghasia zimeongezeka katika eneo tangu utawala huo uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza Oktoba 7 2023.
Takriban Wapalestina 1,102 wameuawa shahidi tangu wakati huo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na karibu wengine 11,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya wanajeshi na walowezi wa Israel katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu.
Wakati huo huo, Wapalestina wasiopungua 21,000 wametiwa nguvu na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi.
Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza Oktoba 2023 na kuuwa shahidi Wapalestina zaidi ya 70,000 kabla ya kufikiwa mapatano ya kusimamisha vita mwezi Okotoba. Israel hadi sasa imekiuka mara kadhaa mapatano hayo ya kusitisha vita iliyofikia kati yake na Hamas.
Kwa miezi kadhaa sasa, mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakitahadharisha kwamba Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wanakabiliwa na vitisho vinavyoongezeka kila uchao vya maangamizi ya kizazi huku hali ya mchafukoge ikiendelea.