
Akizungumza na Shirika la Habari la Ujerumani DPA, Rutte amesema Marekani inatarajia Ulaya ichukue jukumu zaidi na itumie fedha zaidi kwa ulinzi. Na kwamba ana uhakika kabisa kuwa Marekani imewekeza kikamilifu katika NATO. Rutte, amesema mkutano wa NATO wa Juni mjini The Hague ulikuwa hatua muhimu, baada ya washirika wote kukubaliana kuongeza matumizi ya ulinzi hadi asilimia 5 ya pato la taifa (GDP) ifikapo mwaka 2035. Aidha alieleza kuwa makubaliano hayo ni moja ya mafanikio makubwa ya sera za kigeni ya Rais wa Marekani Donald Trump, akisisitiza kuwa ahadi hiyo ya wazi ya kuchangia zaidi inaonyesha mshikamano wa muungano huo katika kuimarisha uwezo wa kijeshi.