Ripota maalum wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kukuza nidhamu ya kidemokrasia na uadilifu kimataifa amesema kuwa, kauli za Waziri wa Vita wa Israel kuhusu kuanzishwa kwa vitongoji vipya katika Ukanda wa Gaza ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

George Katrougalos amesisitiza udharura wa kushughulikia kwa uzito vitendo hivi, akitoa wito wa kuwekwa vikwazo vikubwa dhidi ya utawala wa Kizayuni na kusimamishwa kwa mauzo ya silaha kwa utawala huo.

Pia alibainisha kuwa, kulaani kwa maneno pekee hakutoshi kuzuia ukiukaji wa mara kwa mara wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala wa Israel, na kwamba, jamii ya kimataifa lazima ichukue hatua za kivitendo katika suala hili.

Kaulii hiyo imekuja baada ya Israel Katz Waziri wa Vita wa Israel kusisitiza kuwa Tel Aviv “kamwe haitaondoka ” Gaza, na kwamba watajenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa ukanda huo, hatua ambayo ni kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano.

Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza Oktoba 2023 na kuuwa shahidi Wapalestina zaidi ya 70,000 kabla ya kufikiwa mapatano ya kusimamisha vita mwezi Okotoba. Israel hadi sasa imekiuka mara kadhaa mapatano hayo ya kusitisha vita iliyofikia kati yake na Hamas. 

Kwa miezi kadhaa sasa, mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakitahadharisha kwamba Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wanakabiliwa na vitisho vinavyoongezeka kila uchao vya maangamizi ya kizazi huku hali ya mchafukoge ikiendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *