Leo ni Jumamosi mwezi 6 Rajab 1447 Hijria mwafaka na 27 Disemba 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 964 iliyopita Hassan Sabbah mmoja wa viongozi wakubwa wa Waislamu wa Shia Ismailiya, alitwaa udhibiti wa ngome muhimu na imara ya Alamut, iliyo karibu na mji wa Qazvin, kaskazini mwa Iran. Hassan Sabbah ambaye kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya hapo alikuwa akiwalingania watu kumfuata yeye, aliimarisha utawala wake baada ya kutwaa udhibiti wa ngome hiyo na muda mfupi baadaye alidhibiti miji mingine. Baada ya kudhibiti ngome hiyo ya Alamut, kuliongezeka tabligh (linganio) za kuwataka watu wajiunge na madhehebu ya Shia Ismailiya na wafuasi wa wake walifanya mauaji dhidi ya viongozi wa utawala wa Seljuqi, akiwemo Khoja Nidham al-Mulk. Ngome ya Alamut iliendelea kuwa tegemeo la wafuasi wa Ismailiya nchini Iran hadi pale ilipoangukia mikononi mwa utawala wa Hulagu Khan mwaka 654 Hijiria. Hassan Sabbah alifariki dunia mwaka 518 Hijiria.

Hassan Sabbah

Tarehe 6 Rajab miaka 931 iliyopita, alifariki dunia Abu Muhammad Qasim bin Ali Basri maarufu kwa jina la Ibn Hariri, mwanafasihi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani aliyekuwa akiishi Basra nchini Iraq. Ibn Hariri ndiye mwandishi wa kitabu maarufu cha ‘Maqamaat’ ambacho ni cha aina yake katika taaluma ya fasihi ya Kiarabu. Katika kitabu hicho, Ibn Hariri alieleza siri za fasihi ya lugha ya Kiarabu katika kalibu ya hikaya na semi nyepesi za hekima. 

Miaka 203 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Louis Pasteur, tabibu na mwanakemia wa Kifaransa. Akiwa shuleni Louis Pasteur alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu. 

Louis Pasteur

Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, ulianzishwa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF). Miongoni mwa yaliyokuwa malengo muhimu ya mfuko huo, ni kuandaa nafasi zaidi za ajira, udhibiti wa thamani ya sarafu za kigeni na kuhakikisha kwamba, kunakuweko ukuaji wenye uwiano katika masoko ya kimataifa. Makao Makuu ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa yako mjini New York Marekani. 

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, kufuatia kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, mkataba wa kihistoria wa kuigawa Peninsula ya Korea ulitiwa saini mjini Moscow. Mkataba huo ulitiwa saini na wawakilishi wa nchi tatu za Uingereza, Marekani na Umoja wa Sovieti. Kwa mujibu wa mkataba huo, Peninsula ya Korea ambayo hadi katika zama hizo ilikuwa nchi moja ikagawanywa katika sehemu mbili. Kwa utaratibu huo, kukatokea nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Kusini mgawanyiko ambao ungalipo hadi leo.

Katika siku kama ya leo miaka 18 iliyopita Bi Benazir Bhutto kiongozi wa Chama cha Wananchi cha Pakistan (PPP) aliuawa kwa kufyatuliwa risasi na mlipuko wa bomu uliofanywa na magaidi huko Rawalpindi kaskazini mashariki mwa Pakistan. Mbali na Bi Benazir Bhutto, watu wengine karibu 20 wafuasi wa chama cha PPP waliuawa pia katika mlipuko huo. Bhutto alikuwa Waziri Mkuu wa Pakistan kwa mara ya kwanza mwaka 1988 baada ya kuenguliwa madarakani serikali ya kijeshi iliyokuwa ikiongozwa na Jenerali Muhammad Zia ul Haq.

Bi Benazir Bhutto

Miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha hujuma kubwa na ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Gaza magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wakazi wa eneo hilo waliwakasirisha viongozi wa Kizayuni kutokana na kupambana kwao kishujaa dhidi ya uchokozi na mashambulizi ya Wazayuni na pia hatua yao ya kuiunga mkono serikali halali ya Palestina iliyokuwa ikiongozwa na harakati ya Hamas. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ukanda wa Gaza ukawekwa chini ya mzingiro wa kiuchumi wa utawala haramu wa Israel kwa karibu mwaka moja na nusu kabla ya mashambulizi hayo, mzingiro ambao unaendelea kuwasababishia Wapalestina wa eneo hilo matatizo chungu nzima kama vile ukosefu wa chakula na dawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *