Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, amesisitiza ujumbe huo mapema mwaka huu mjini Geneva na kuuliza swali mbele ya Baraza la Haki za Binadamu:
“Je, tunachukua hatua zinazohitajika kuwalinda watu dhidi ya machafuko ya tabianchi, kulinda mustakabali wao na kusimamia rasilimali za asili kwa njia inayoheshimu haki za binadamu na mazingira?”
Jibu lake lilikuwa rahisi sana: hatufanyi vya kutosha.
Katika muktadha huo, athari za mabadiliko ya tabianchi lazima zieleweke si tu kama dharura ya tabianchi, bali pia kama ukiukwaji wa haki za binadamu, Profesa Joyeeta Gupta ameiambia UN News hivi karibuni.
Profesa Gupta ni mwenyekiti mwenza wa chombo cha kimataifa cha ushauri wa kisayansi, Earth Commission, na ni mmoja wa wawakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs.
Nani anaathirika zaidi?
Profesa Gupta amesema kuwa Mkataba wa Tabianchi wa mwaka 1992 haukukadiria madhara kwa binadamu.
Amebainisha kuwa Mkataba wa Paris ulipopitishwa mwaka 2015, makubaliano ya kimataifa yaliweka lengo la kudhibiti ongezeko la joto hadi nyuzi joto 2 za Selsiasi, baadaye ikatambuliwa kuwa nyuzi joto 1.5 za Selsiasi ni lengo salama zaidi.
Hata hivyo, kwa nchi ndogo za visiwa vinavyoendelea, hata lengo hilo lilikuwa ni muafaka uliolazimishwa na ukosefu wa usawa wa madaraka, na kwamba “kwao, nyuzi joto mbili hazikuwa zinakubalika kwa kuishi,” amesema Profesa Gupta.
“Kuongezeka kwa kina cha bahari, kuingia kwa maji ya chumvi, na dhoruba kali kunatishia kufuta kabisa mataifa hayo. Nchi tajiri zilipodai uthibitisho wa kisayansi, Jopo la Kiserikali la Mabadiliko ya Tabianchi IPCC, lilipewa jukumu la kuchunguza tofauti kati ya nyuzi joto 1.5 na 2 za Selsiasi,” ameendelea.
Amesema matokeo yalikuwa wazi, nyuzi joto 1.5 ni hatarishi kidogo ikilinganishwa na 2, lakini bado ni hatari.
Katika utafiti wake mwenyewe uliochapishwa kwenye jarida la Nature, anasema kuwa nyuzi joto 1 ni mpaka wa haki, kwa sababu kuvuka kiwango hicho kunasababisha athari za mabadiliko ya tabianchi kukiuka haki za zaidi ya asilimia moja ya watu duniani abao ni takribani watu milioni 100.
Janga kubwa, amebainisha, ni kwamba dunia ilivuka nyuzi joto 1 mwaka 2017, na kuna uwezekano mkubwa wa kuvuka nyuzi joto 1.5 ifikapo mwaka 2030.
Amesisitiza kuwa ahadi za kupunguza joto baadaye katika karne hii zinapuuza uharibifu usioweza kurekebishwa, ikiwemo kuyeyuka kwa barafu za milele, kuporomoka kwa mifumo ya ikolojia, na kupotea kwa maisha ya watu.
“Ikiwa barafu za Himalaya zitayeyuka,” amesema, “hazitarudi tena. Tutaishi na matokeo yake milele.”
Mwanamume akimsaidia mwanamke baada ya gari lake kukwama kwenye maji yanayofika kiunoni. Mvua duniani inazidi kuwa baya zaidi kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Suala la uwajibikaji
Haki ya tabianchi na maendeleo vinaenda sambamba. Kila haki ya msingi — kuanzia maji na chakula hadi makazi, usafiri na umeme vinahitaji nishati.
“Kuna imani kwamba tunaweza kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu bila kubadilisha namna watu matajiri wanavyoishi. Hilo halifanyi kazi kihesabu wala kimaadili,” Profesa Gupta ameeleza.
Utafiti wake unaonesha kuwa kukidhi mahitaji ya msingi ya binadamu kuna alama kubwa ya uzalishaji wa hewa chafuzi.
Utafiti huo pia unaonesha kuwa, kwa kuwa dunia tayari imevuka mipaka salama, jamii tajiri lazima zipunguze uzalishaji wa hewa ukaa kwa kasi zaid si tu kulinda tabianchi, bali pia kuunda nafasi ya hewa ukaa kwa wengine kutimiza haki zao.
“Kushindwa kufanya hivyo kunageuza ukosefu wa usawa kuwa dhuluma,” amesisitiza.
Mabadiliko ya tabianchi na kuhama kwa watu
Kuhama kwa watu ni mojawapo ya athari zilizo wazi zaidi za dhuluma ya tabianchi. Hata hivyo, sheria za kimataifa bado hazitambui rasmi wakimbizi wa tabianchi.
Profesa Gupta anaeleza mchakato huo kwa uwazi:
“Mabadiliko ya tabianchi kwanza hulazimisha watu kujirekebisha kwa mfano, kubadili kutoka kilimo cha mpunga kinachohitaji maji mengi kwenda mazao yanayostahimili ukame. Marekebisho yanaposhindikana, watu hupata hasara za ardhi, riziki, usalama. Wakati uhai wenyewe unapokuwa hauwezekani, ndipo uhamaji huanza,” amesema.
“Ikiwa ardhi inakuwa kavu kiasi kwamba haiwezi kuzalisha chakula na hakuna maji ya kunywa,” amesema, “watu hulazimika kuondoka.”
Ameongeza kuwa uhamaji mwingi unaosababishwa na tabianchi leo hutokea ndani ya nchi au kanda, si kuvuka mabara.
“Kuhama ni gharama kubwa, ni hatari, na mara nyingi hakutakiwi. Changamoto ya kisheria iko katika kuthibitisha sababu, Je, watu waliondoka kwa sababu ya tabianchi, au kwa sababu ya mambo mengine kama utawala mbovu au kushindwa kwa masoko?”
Amebainisha kuwa “Hapa ndipo sayansi ya uhusiano wa sababu inakuwa muhimu. Tafiti mpya sasa zinachambua data za miongo kadhaa kuonesha lini na vipi mabadiliko ya tabianchi yanabadilisha mvua, joto, afya na matukio ya hali mbaya ya hewa. Kadri sayansi hii inavyoendelea, huenda ikawezekana kujumuisha uhamaji wa tabianchi katika sheria za kimataifa za wakimbizi”.
Hiyo, amesema, “ndiyo hatua inayofuata.”
Watoto barani Afrika ni miongoni mwa walio katika hatari zaidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mfumo wa kisheria uliovunjika
Profesa Gupta amesema kuwa madhara ya tabianchi yamekuwa magumu kushughulikiwa kupitia sheria za haki za binadamu kutokana na mgawanyiko wa mfumo wa sheria za kimataifa.
“Mgawanyiko huu unaruhusu Mataifa kugawanya wajibu. Wanaweza kusema, nimekubaliana na hili hapa, lakini si pale,’” amesema.
“Mikataba ya mazingira, makubaliano ya haki za binadamu, mikataba ya biashara, na mifumo ya uwekezaji vinafanya kazi katika ulimwengu unaojitegemea. Nchi zinaweza kusaini makubaliano ya tabianchi bila kufungwa na mikataba ya haki za binadamu, au kulinda wawekezaji huku zikipuuzia uharibifu wa mazingira,” ameongeza.
Amesema hali hii ndiyo sababu imekuwa vigumu sana kuitaja tabianchi kama ukiukwaji wa haki za binadamu katika ngazi ya kimataifa. Hadi hivi karibuni, madhara ya tabianchi yalijadiliwa kwa lugha ya kiufundi sehemu kwa milioni ya hewa ukaa, malengo ya joto, njia za uzalishaji bila kuuliza wazi, hii inawafanyia nini watu?. Hivi karibuni tu hali hiyo imeanza kubadilika.
Katika maoni ya kihistoria ya ushauri, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ilifafanua kuwa mabadiliko ya tabianchi hayawezi kutathminiwa kwa kujitenga. Mahakama na serikali, ICJ ilisema, lazima zizingatie wajibu wa tabianchi pamoja na haki za binadamu na mikataba mingine ya mazingira.
Kwa Profesa Gupta, mabadiliko haya ya kisheria yamechelewa sana lakini ni muhimu.
“Hatimaye inawaambia serikali, huwezi kuzungumzia tabianchi bila kuzungumzia watu.”
Mabadiliko ya tabianchi hayana mipaka
Kuweka wajibu wa mabadiliko ya tabianchi ni suala tata sana kwa sababu athari zake huvuka mipaka, amesema.
“Kwa mfano, mkulima kutoka Peru alishitaki kampuni ya Kijerumani katika mahakama ya Ujerumani kwa uharibifu uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Mahakama ilikubali kuwa walalamikaji wa kigeni wanaweza kufungua kesi kama hizo, lakini kuthibitisha uhusiano kati ya uzalishaji wa hewa chafuzi na madhara bado ni changamoto kubwa. Kesi hii inaonesha ugumu wa kuwawajibisha Mataifa au makampuni kwa madhara ya haki za binadamu yanayohusiana na tabianchi yanayovuka mipaka,” ameongeza.
Profesa Gupta amesema sayansi ya uhusiano wa sababu sasa inafanya iwezekane kuunganisha uzalishaji wa hewa chafu na madhara mahususi.
ICJ sasa imethibitisha kuwa matumizi yanayoendelea ya mafuta ya kisukuku yanaweza kuhesabiwa kama kitendo batili chini ya sheria za kimataifa.
Mataifa yanawajibika si tu kwa uzalishaji wao, bali pia kwa kudhibiti makampuni yaliyo ndani ya mipaka yao.
Moshi wa magari, jenereta za dizeli na kuchoma taka na samadi vimesababisha uchafuzi wa hewa kwenye mij wa Lagos nchini Nigeria kama inavyoonekana kwenye picha hii ya mwaka 2016
“Mikakati tofauti ya kisheria inaibuka, kuanzia mashitaka dhidi ya upotoshaji wa taarifa za makampuni nchini Marekani hadi sheria ya Ufaransa ya uangalizi wa makampuni,” ameongeza.
Utulivu wa tabianchi kama haki ya pamoja ya binadamu
Badala ya kuangalia tabianchi kama haki ya mtu mmoja mmoja, Profesa Gupta anapendekeza itambuliwe kama haki ya pamoja ya kuwa na tabianchi thabiti.
Ameeleza kuwa utulivu wa tabianchi unaendeleza kilimo, mifumo ya maji, minyororo ya usambazaji, na kutabirika kwa maisha ya kila siku na bila huko, jamii haiwezi kufanya kazi.
“Tabianchi hufanya kazi kupitia maji,” amesema. “Na maji yako katikati ya kila kitu.”
Mahakama kote duniani zinazidi kutambua kuwa kutokuwa na utulivu wa tabianchi kunadhoofisha haki zilizopo za binadamu, hata kama tabianchi yenyewe bado haijatambuliwa rasmi kama haki.
Mtazamo huu sasa unaakisiwa katika ngazi za juu kabisa za Umoja wa Mataifa.
Kudhoofika kwa haki za msingi
Akizungumza mbele ya Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva mwezi Juni mwaka huu, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, alionya kuwa mabadiliko ya tabianchi tayari yanadhoofisha haki za msingi, hasa kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi.
Hata hivyo, pia alielezea hatua za kukabiliana na tabianchi kama fursa.
“Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuwa kichocheo chenye nguvu cha maendeleo,” alisema, ikiwa dunia itajitolea katika mpito wa haki kutoka mifumo inayoharibu mazingira.
“Kile tunachohitaji sasa,” alisisitiza, “ni ramani ya kufikiria upya jamii zetu, uchumi wetu na siasa zetu kwa njia ya haki na endelevu.”
Mabadiliko ya tabianchi yameongeza hatari ya hali ya hewa kavu, ya joto ambao inachangia kuchochea moto wa nyika
Dhamira ya kisiasa, nguvu na uwajibikaji
“Kudhoofika kwa mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, unaoonekana kupitia kujiondoa mara kwa mara kwa Marekani kwenye Mkataba wa Paris, kumeathiri imani ya kimataifa. Wakati huohuo, asilimia 70 ya upanuzi mpya wa matumizi ya mafuta ya kisukuku unaendeshwa na nchi nne tajiri, Marekani, Canada, Norway na Australia,” amesema Profesa Gupta.
Anasema itikadi ya kibepari huria inayolenga masoko, kupunguza udhibiti na uhuru wa mtu binafsi haiwezi kutatua mgogoro wa pamoja.
“Mabadiliko ya tabianchi ni tatizo la manufaa ya umma,” amesema. “Yanahitaji sheria, ushirikiano na Mataifa yenye nguvu.”
Nchi zinazoendelea zinakabiliwa na mtanziko, kusubiri fedha za tabianchi huku uzalishaji wa hewa chafu ukiendelea kuongezeka, au kuchukua hatua zenyewe na kutafuta haki baadaye. Kusubiri, anaonya, ni sawa na kujiua.
Kama Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa alivyohitimisha mjini Geneva, mpito wa haki lazima usimwache mtu yeyote nyuma.
“Ikiwa tutashindwa kulinda maisha, afya, ajira na mustakabali,” Volker Türk alionya, “tutarudia zile dhuluma tunazodai kupambana nazo.”