Chanzo cha picha, TTB/Insta
Muda wa kusoma: Dakika 5
Kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ni heshima kubwa. Ni kama harusi ya kitaifa, sherehe ya mafanikio baada ya safari ndefu ya ushindani, uchungu na matumaini.
Ndiyo maana kwa mataifa ambayo hayajawahi kufuzu AFCON kabisa, zaidi ya nchi 10 barani Afrika, kushiriki mashindano haya hubaki kuwa ndoto. Tanzania na Uganda wameifikia hatua hiyo. Wote wapo kwenye sherehe, wapo kwenye harusi. Lakini si kila harusi huishia kwa furaha.
Jumamosi hii, Desemba 27, kwenye Stade El Barid, Rabat, sherehe hiyo inaweza kugeuka kuwa msiba. Tanzania na Uganda wanakutana kwa mara ya kwanza kabisa katika fainali za AFCON, katika dabi ya Afrika Mashariki ambayo mshindi ataondoka akiwa na matumaini mapya ya kufuzu hatua ya 16 bora, huku aliyeshindwa akibaki akitazama kaburi la ndoto yake.
Hii ndiyo maana ya dabi ya msiba harusini, furaha kwa mmoja, msiba kwa mwingine, na uchungu unaoongezwa na ukweli kwamba anayekuondoa si adui wa mbali, bali ni ndugu.
Hivyo, hii si mechi ya alama tatu tu, ni mechi ya hisia ya undugu wa kiushindani, historia, na heshima ya kanda.
Tanzania kuanzisha tumaini au msiba?
Chanzo cha picha, CAF
Kwa takwimu za juu juu, Tanzania inaingia kwenye dabi hii ikiwa dhaifu. Taifa Stars hawajawahi kushinda mechi yoyote katika historia yao ya AFCON, wakicheza mechi 10, kutoa sare tatu na kupoteza saba. Kipigo cha 2–1 dhidi ya Nigeria kwenye mchezo wa ufunguzi kilikuwa ni kipigo chao cha saba katika mashindano haya, na pia kiliendeleza mfululizo wa kufungwa katika michezo ya AFCON waliowahi kucheza. Sare mbili ya 1-1 dhidi ya Zambia na ile ya 0–0 dhidi ya DR Congo mwaka 2023, zilikuwa za matumaini kwa kiasi.
Lakini takwimu hizo zikisomwa kwa undani, Tanzania haiko mbali kabisa na ushindani. Licha ya kutoshinda, Taifa Stars wamefunga mabao katika mechi sita kati ya 10 za AFCON walizocheza. Bao dhidi ya Nigeria lilimaanisha kuwa Tanzania sasa imefunga angalau bao moja katika kila toleo la AFCON waliloshiriki. Charles M’Mombwa, aliyefunga dhidi ya Super Eagles, sasa amehusika katika mabao matatu kati ya manne ya mwisho ya Tanzania katika mashindano yote, akionyesha kuwa anaibuka kama mhimili mpya wa mashambulizi.
Katika mchezo dhidi ya Nigeria, Tanzania waliruhusu mashuti 11 yaliyolenga lango, lakini walijibu kwa mashuti matatu yaliyolenga lango la wapinzani. Kipa Zuberi Foba, licha ya kufungwa mabao mawili, aliokoa mipira minane, idadi ya tatu kwa wingi zaidi kwa mlinda mlango yeyote katika raundi ya kwanza kwenye mechi za makundi. Hii inaashiria kwamba ingawa ulinzi wa Tanzania unapwaya, bado unajengwa na msingi wa kupambana.
Kiufundi, uamuzi wa kumtumia Novatus Miroshi kama kiungo mkabaji dhidi ya Nigeria ulileta uwiano mzuri. Akiungana tena na Alphonce Msanga, Tanzania itajaribu kudhibiti eneo la kati na kuvunja mashambulizi ya Uganda. Kumkosa kiungo mahiri Feisal Salum Abdallah katika mechi iliyopita haikuonekana sana pengo kwa namna viungo hawa wawili walivyocheza, lakini akirejea Feisal uzoefu wake utamaanisha nguvu nyingine kwa Stars dhidhi ya The Cranes.
Ushindi wa Tanzania hapa hautakuwa tu ushindi wa kwanza wa AFCON utakuwa mwanzo wa tumaini jipya. Lakini kipigo? Kitakuwa msiba mzito, kwa sababu kitatoka mikononi mwa jirani.
Uganda historia inawabeba
Chanzo cha picha, CAF
Uganda wanaingia kwenye mechi hii wakiwa na uzito mkubwa wa historia ya AFCON. Kipigo cha 3–1 dhidi ya Tunisia kilikuwa ni cha 17 kwa Cranes katika mechi 24 walizowahi kucheza AFCON. Pia kiliendeleza rekodi mbaya ya Uganda ya kupoteza michezo ya ufunguzi, wakifanya hivyo mara tano katika nane walizowahi kushiriki.
Tanzania imepoteza kila mchezo wa ufunguzi wa michuano ya AFCON, Uganda wao imepoteza kwenye michezo ya pili ya makundi. Tangu mfumo wa makundi ulipoanzishwa mwaka 1968, Uganda hawajawahi kushinda mchezo wa pili wa kundi. Wamepoteza mara nne na kutoa sare mara mbili. Mara tatu waliwahi kupoteza michezo miwili ya kwanza ya kundi mwaka 1962, 1968 na 1976 na mara zote waliondolewa mapema.
Hata hivyo, kuna ishara ndogo ya matumaini. Bao la Denis Omedi dhidi ya Tunisia lilifungwa dakika ya 91 na sekunde 25, likiwa ndilo kama bao ahueni zaidi kwa Uganda AFCON. Bao hilo lilivunja ukame wa dakika 376 bila kufunga, likionyesha kuwa The Cranes bado wana uwezo kukumaliza, hasa katika nyakati za mwisho.
Ukiacha DRC, Uganda ni timu bora kwa ukanda wa Afrika Mashariki, na kwa sababu mara nyingi hupata matokeo mazuri dhidi ya jirani yake Tanzania, mchezo huu itawaongezea tumaini, kwa sababu ina uhakika zaidi wa kupata alama, kuliko dhidi ya Nigeria, mchezo wao wa mwisho wa kundi. Hali hiyo pia iko kwa Tanzania, wanajuana na ndugu zao, hawajapishana sana, lolote linaweza kutokea kama wakicheza kwa adabu kama walivyofanya dhidi ya Nigeria.
Takwimu muhimu za ndugu wenye ‘uhasama’
Chanzo cha picha, CAF
‘Uhasama’ kati ya Tanzania na Uganda una historia ndefu, ukiwa ulianza rasmi mwaka 1964, pale Tanzania ilipoifunga Uganda kwa mabao 3–0 katika michuano ya Kombe la Afrika Mashariki. Hata hivyo Uganda ilikuja kulipiza kiasi kwa rekodi ya ushindi mnono wa mabao 5-0, ilikuwa Novemba 1991, ikatika mashindano ya Kombe la CECAFA.
Katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Uganda imewahi kukutana mara mbili na wapinzani kutoka Afrika Mashariki, na imepoteza mechi zote mbili ikifungwa 2–1 na 2–0 dhidi ya Ethiopia katika hatua ya makundi ya mashindano ya mwaka 1968 na 1976.
Kwa upande wa Tanzania, mechi yao pekee ya AFCON dhidi ya mpinzani wa Afrika Mashariki ilimalizika kwa kipigo cha mabao 3–2 dhidi ya Kenya katika mchezo wa pili wa kundi kwenye fainali za mwaka 2019.
Zaidi ya hayo, baadhi ya wachezaji wa Uganda wana uhusiano wa karibu na soka la Tanzania. Viungo Khalid Aucho na Steven Mukwala wanacheza soka lao la klabu nchini Tanzania, wakiitumikia Singida Black Stars na Simba SC mtawalia. Aucho pia anafundishwa katika ngazi ya klabu na kocha wa sasa wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, hali inayoongeza ladha ya kipekee katika dabi hii ya Afrika Mashariki.
Ukiacha hilo, Kwa Tanzania, ikipata bao mchezo wa leo litawaweka kwenye historia ya kufunga katika michezo miwili mfululizo ya AFCON kwa mara ya kwanza tangu 1980. Kwa Uganda, kushindwa kutakuwa pigo kubwa kabla ya kukutana na Nigeria kwenye mchezo wa mwisho wa kundi.
Pia katika historia ya kukutana wao kwa wao, Uganda wana faida kubwa dhidi ya Tanzania katika mechi 61, imepata ushindi mara 33, sare 16 na Tanzania wakipata ushindi mara 12 pekee. Lakini historia ya karibu inawaumbua kiasi Uganda, Tanzania ilishinda mechi zote mbili za kufuzu AFCON 2023 kwa matokeo ya 1–0. Hivyo, Uganda wanabeba historia ya zamani, lakini Tanzania wanabeba kumbukumbu za karibuni.
Ndiyo maana hii ni dabi ya msiba harusini. Kuna harusi, lakini kunaweza kutokea msiba, msiba utakaosababishwa na ndugu yako. Mmoja ataendelea kucheza muziki wa harusi, mwingine ataanza kuhesabu gharama za mazishi ya ndoto yake kama mmoja atafungwa. Lakini cha kuumiza zaidi, ni kwamba anayekutoa kwenye sherehe si mgenim, bali ni ndugu yako wa Afrika Mashariki. Zikitoka sare, huzuni inaweza kuongezeka zaidi Afrika Mashariki, kwani matokeo ya mchezo wa Nigeria vs Tunisia yanaweza kubainisha uzito wa msiba huo Afrika Mashariki.