Mwanamume mmoja ameketi kwenye ukingo wa jengo lililoharibiwa katika kitongoji cha Al-Saftawi, magharibi mwa jiji la Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza mnamo Desemba 10, 2025.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    • Author, By Muhannad Tutunji
    • Nafasi, BBC News Arabic
    • Akiripoti kutoka, Jerusalem
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Israel na Hamas zilifikia makubaliano ya awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano huko Gaza mwezi Oktoba, chini ya usimamizi wa Marekani. Makubaliano hayo yalizua matumaini kwamba yangekuwa hatua ya kuelekea kumaliza mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Hata hivyo, miezi miwili baadaye, hali haijabadilika kwa kiasi kikubwa. Gaza bado iko katika awamu ya kwanza ya makubaliano, ikiwa imegawanyika kati ya pande zinazokinzana. Wakazi wengi wameyakimbia makazi yao na wanaendelea kuishi katika mazingira ya uharibifu mkubwa.

Katika awamu ya pili ya mpango huo, uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump, pande zote mbili zinakabiliwa na maamuzi mazito ya kisiasa na kiusalama. Hamas inatakiwa kukabidhi silaha zake, huku Israel ikipaswa kupunguza uwepo wake wa kijeshi Gaza na kuhamisha majukumu ya usalama kwa kikosi cha kimataifa cha kudumisha utulivu. Aidha, suala la kuundwa kwa serikali ya mpito ya kusimamia Gaza, pamoja na hatma ya mateka wa mwisho wa Israel, Ran Gvili, bado halijapatiwa suluhu.

Hatma ya mateka wa mwisho wa Israel

Ran Gvili akiwa amevalia sare za polisi - alikuwa na umri wa miaka 24 wakati wa shambulio la Hamas, tarehe 7 Oktoba 2023.

Chanzo cha picha, Handout

Ran Gvili, afisa wa polisi wa Israel, alitekwa wakati wa mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba. Kwa mujibu wa Hamas, juhudi za kumtafuta katika vifusi vya Gaza bado hazijazaa matunda.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesisitiza kuwa Hamas lazima irejeshe mateka wote, walioko hai au waliokufa, kabla makubaliano hayo kuendelea hadi awamu ya pili.

Wazazi wa Gvili waliarifiwa mwaka jana kwamba mwana wao aliaga.

Talik, ambaye ana nywele nyeusi kwenye mkia wa farasi na amevaa miwani yenye rim nyeusi, anapiga picha na mume wake Itzik, ambaye ana nywele fupi za kijivu na ndevu na amevaa cheni ya fedha. Wote wawili wana maneno ya upande wowote.

“Waliiba mtoto wetu, wakamwiba,” mamake Talik aliambia BBC News. “Wanajua alipo,” babake Itzik alisema. “Wanajaribu tu kumficha au kumweka. Wanacheza [na] nasi.”

Hamas imekanusha madai hayo na kuituhumu Israel kwa kukwepa utekelezaji wa makubaliano. Pamoja na mvutano huo, vyombo vya habari vya Israel vinaripoti kuwa Marekani ina nia ya kuhimiza kwa nguvu mpito kuelekea awamu ya pili.

Mjadala huo uliungwa mkono na Gershon Baskin, mpatanishi wa zamani wa Israel katika masuala ya mateka, ambaye alieleza BBC News Africa kuwa Israel haina mbinu nyingi za kuendelea kuchelewesha awamu ya pili, kwani uamuzi wa kisiasa kutoka Washington tayari umefanyika.

Baskin, ambaye hapo awali amekuwa na jukumu muhimu katika njia zisizo rasmi za mawasiliano kati ya Israel na Hamas, aliongeza kuwa suala la mwili wa mateka kubaki Gaza “sio sababu tosha” kuchelewesha kuanza kwa awamu ya pili.

Soma pia:

Changamoto ya kuvua silaha Hamas

Kuvua silaha Hamas kunachukuliwa kuwa kikwazo kikubwa zaidi cha utekelezaji wa awamu ya pili ya usitishaji mapigano. Pendekezo la kuanzishwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Kudumisha Utulivu limeibua mjadala mkubwa, hasa kutokana na msimamo wa Israel wa kupinga ushiriki wa Uturuki, msimamo unaoungwa mkono na Marekani.

Hadi sasa, hakuna nchi iliyothibitisha rasmi kushiriki katika kikosi hicho. Kwa upande wake, Hamas imeashiria kuwa inaweza kukubali kuhifadhi silaha zake au kuzikabidhi kwa chombo cha Kipalestina au upande wa tatu, lakini si kwa Israel wala Marekani.

Marekani inatambua kuwa suala la kuvua silaha Hamas linahusiana moja kwa moja na kuondoka kamili kwa wanajeshi wa Israel Gaza, jambo linalozidi kuwa gumu kutekelezwa huku majeshi hayo yakiendelea kuwepo ndani ya eneo hilo.

Majeshi ya Israel yataondoka kwenda wapi?

Kwa sasa, Israel inadhibiti zaidi ya nusu ya Ukanda wa Gaza asilimia 53%. Katika awamu ya kwanza ya makubaliano, ilikubali kujiondoa hadi mstari maalumu wa mpaka unaozunguka kaskazini, kusini na mashariki mwa Gaza, unaojulikana kama “Mstari wa Njano”.

A map of Gaza showing the yellow line, behind which Israeli forces have withdrawn

Awamu ya pili inahitaji makubaliano mapya kuhusu mipaka ya uwepo wa kijeshi wa Israel, taratibu za ulinzi, ujenzi upya wa Gaza, pamoja na ufuatiliaji wa kimataifa. Masuala haya ni nyeti kwani yanaathiri usalama wa miji ya Israel iliyo mpakani na Gaza na mustakabali wa eneo la Philadelphi, lililo kando ya mpaka wa Gaza na Misri.

Kwa mujibu wa Jenerali mstaafu Israel Ziv, pande zote mbili zinaonesha kusita kusonga mbele.

”Hamas inaogopa kupoteza udhibiti wake, huku uongozi wa Israel ukikabiliwa na shinikizo la kisiasa la ndani linaloifanya isitake kujiondoa haraka.” aliiambia BBC News.

Gen Ziv anaamini kuwa mtu ambaye anaweza kushinikiza pande zote mbile kuingia awamu ya pili ni Rais wa Marekani Donald Trump na muda unampa kisogo.

“Kwa kusubiri nadhani tutakosa fursa ya maafikiano kwani Hamas wanajipanga upya na kujitayarisha kurejea kudhibiti Gaza,” anaeleza.

Ni nani ataiongoza Gaza?


Wapalestina ambao hawana makazi wanatembea katikati ya vifusi wakirejea kwa makazi yao yaliyoko al-Zahra kaskazini mwa kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati ya ukanda wa Gaza mwezi Oktoba 14, 2025 baada yausitishaji mapigano kuanza.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Kuundwa kwa utawala wa mpito wa Gaza baada ya Hamas ni changamoto nyingine muhimu. Ingawa mpango unaelekeza kuundwa kwa serikali huru ya wataalamu wa Kipalestina, Israel ina wasiwasi kwamba Hamas au Mamlaka ya Palestina inaweza kuendelea kuwa na ushawishi ndani ya mfumo huo.

Hapo awali mamlaka hiyo ilikuwa na udhibiti mdogo wa sehemu za Gaza na Ukingo wa Magharibi, lakini tangu Hamas ilipoiteka Gaza mwaka 2007, imetawala sehemu tu za Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel.

Serikali ya Netanyahu inapinga ushiriki wa Hamas na Mamlaka ya Palestina, ikisisitiza kuwa Gaza inapaswa kuongozwa na chombo huru kisichoegemea upande wowote. Aidha, Israel ina hofu kwamba awamu ya pili ya makubaliano inaweza kufungua njia ya kuanzishwa kwa taifa la Palestina sambamba na Israel.

Haya ni kwa mujibu wa Gershon Baskin, mpatanishi wa zamani wa Israel.

Ni nini kiko mezani katika mazungumzo ya Netanyahu-Trump?

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin (kushoto) akizungumza na Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa mkutano katika Ofisi ya Oval ya White House Aprili 7, 2025 huko Washington.

Chanzo cha picha, Getty Images

Masuala haya muhimu yanatarajiwa kujadiliwa katika mkutano kati ya Netanyahu na Trump huko Florida baadaye mwezi huu.

Rais wa Marekani, ambaye aliongoza usitishaji vita huko Gaza, anatazamiwa kutangaza uanachama wa Bodi mpya ya Amani ya Gaza mapema mwaka ujao.

Netanyahu anatarajiwa kushinikiza kuvuliwa silaha kwa Hamas, kuzuia ushiriki wake katika utawala wa Gaza, kudumisha uwepo wa kijeshi wa Israel katika maeneo yanayojulikana kama Buffer, na kuzuia kupelekwa kwa wanajeshi wa Uturuki.

Kwa upande mwingine, Trump anaweza kumhimiza Netanyahu kuheshimu kikamilifu makubaliano ya usitishaji mapigano, akidai kuwa ukiukwaji mwingi umetoka upande wa Israel.

Tangu kuanza kwa usitishaji mapigano tarehe 7 Oktoba, mamia ya Wapalestina wameuawa na maelfu kujeruhiwa, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza. Jumla ya waliopoteza maisha tangu vita kuanza Oktoba 2023 imefikia zaidi ya watu 70,665, huku majeruhi wakizidi 171,145.Idadi hii inajumuisha hadi tarehe 15 mwezi Desemba 2025.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *