MWENYEKITI wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Mkoa wa Dodoma, Mchungaji Eliya Mathayo amewaomba wazazi na walezi kushirikiana na serikali kuhakikisha watoto wote walioandikishwa kuanza elimu ya msingi wanapelekwa kuanza masomo shule zikifunguliwa Januari mwakani.
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika kanisani hapo.
Alisema kila mtoto ana haki na fursa ya kupata elimu na serikali imefanya jitihada kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya shule kuhakikisha watoto wengi wanaifikia fursa.
Aidha, aliwataka wazazi kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza wanaripoti shuleni ili kuanza masomo.
“Fursa za elimu zipo wazi kwa watoto wote, hivyo niwaombe wazazi na walezi wasikae na watoto majumbani hata kama ni walemavu,” alisema.
Alisema elimu ndiyo msingi mkubwa wa watoto kwenye maisha na itawawezesha kuondokana na utegemezi na hatimaye kujisimamia na kujitegemea wenyewe.
Mchungaji Mathayo, ambaye pia ni msimamizi wa Kanisa la Free Pentecostal Church Tanzania la Area A mkoani Dodoma, alisema serikali kwa asilimia kubwa imetatua changamoto za miundombinu ya majengo yake na kila eneo kuanzia kwenye vitongoji, vijijini, kata hadi wilayani kuna shule, kwa maana hiyo ni makosa makubwa kuwaacha watoto hao majumbani.
“Hivyo nishauri wazazi na walezi wasiwaweke na kuwaficha watoto hao majumbani, ukizingatia kuwa elimu inaleta maarifa ufahamu, kwa maana hiyo watoto wenye sifa ya kuanza kusoma wapelekwe shule, wawe walemavu ama wasiwe walemavu,” alisema.
Aidha, aliwataka wazazi kuhakikisha wanashirikiana na walimu kuhakikisha watoto wanapata uelewa wa elimu, badala ya suala hilo kuwaachia watoto peke yao bila kupata msaada wowote wa kitaaluma.
