MWAKA 2025 unamalizika na hivi karibuni tunaukaribisha Mwaka Mpya wa 2026.
Ni desturi ya wengi kuwa na shamrashamra za hapa na pale kuukaribisha Mwaka Mpya, siku ya mkesha ni Desemba 31 saa 6:00 usiku kwa watu hupiga madebe na kupeana hongera kwa kumaliza mwaka.
Kwenye michezo, mwaka 2025 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa kufanya vizuri, yaani ulikuwa mwaka wa neema baada ya wachezaji wetu kujituma na kupata matokeo mazuri.
Kwa ujumla mwaka 2025 ulikuwa na mafanikio makubwa katika michezo mbalimbali kuanzia soka, ambayo iliandaliwa kwa mafanikio makubwa ikiwemo mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024), ambayo iliandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Uganda na Kenya.
Mwaka 2026 uwe na mafanikio zaidi kwa mashirikisho na vyama vya michezo nchini kufanya juhudi zaidi kuendeleza michezo kuanzia ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Kwa wale ambao hawajafanya vizuri, mwaka 2026 uwe wa kujirekebisha na kuangalia waliangukia wapi ili wasije wakarudia tena makosa yaleyale na wale waliofanya vizuri tunashauri lazima waendeleze mazuri waliyofanya.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa tayari kusaidia michezo na mwaka unaoisha ilitenga bajeti kubwa kwa ajili ya michezo yote ili mradi mashirikisho yaeleze yatatumiaje fedha hizo kwa maendeleo ya michezo.
Fedha hizo sio za kila mtu, ila zinatakiwa kutumika kwa jinsi zilivyopangiwa na viongozi wa michezo watakaozitumia kiholela wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Mwaka 2025 mchezo wa soka ulionekana kama ndio umefaidika zaidi lakini tunaamini michezo mingi imefainika ila wengine mipangilio ya kiutekelezaji na utendaji pengine iliwaangusha.
Tunashauri mashirikisho mengine ya michezo nchini kuwa na mpangilio mzuri, yaani kuomba fedha na kuzielekeza katika matumizi sahihi kwa maendeleo ya mchezo husika.
Tatizo kubwa la viongozi wa mashirikisho mengi ya michezo wanashindwa kuwa na mpango mkakati wa maendeleo ya michezo yao, ndiyo maana wanakosa fedha na wakati mwingine wanakosa ufadhili.
Wengine wanaogopa hata kuomba fedha hizo na ndiyo maana wanashindwa kuzipata au wengine hata kueleza watazitumiaje.
Hivyo tunashauri mwaka ujao uwe wa mafanikio zaidi kuliko huu unaoelekea kumalizika, hivyo viongozi wasikae kimya na ikibidi watumie wataalamu ili kuandikia andiko la maendeleo ya mchezo husika.
Aidha, tunawiwa kusema mwaka ujao uwe wa mafanikio makubwa katika michezo yote nchini, hivyo kupeperusha vyema Bendera ya Tanzania kimichezo ndani na nje ya nchi.
