
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema mashambulio makubwa ya jeshi la Marekani na mwanaharamu wake katika eneo la Magharibi mwa Asia yalishindwa kutokana na ubunifu, ushujaa na kujitolea kwa vijana wa Iran ya Kiislamu.
Katika ujumbe wake kwa mkutano wa 59 wa kila mwaka wa Umoja wa Jumuiya za Wanafunzi wa Kiislamu barani Ulaya mapema leo Jumamosi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameangazia jukumu la vijana wa Iran katika kuzima mashambulizi makubwa ya jeshi la Marekani na “kitoto chake cha kuaibisha” katika eneo hilo, akimaanisha utawala haramu wa Israel.
“Wapendwa Vijana! Mwaka huu, nchi yenu, kutokana na imani, umoja na kujiamini, imepata hadhi na uzito mpya duniani. Uvamizi mkubwa wa jeshi la Marekani na kijitoto chake cha kuaibisha katika eneo hili ulishindwa kutokana na ubunifu, ushujaa na kujitolea kwa vijana wa Iran ya Kiislamu”, umesema ujumbe wa Ayatullah Khamenei.
Ameongeza kuwa: Imethibitishwa kwamba taifa la Iran, kwa kutumia uwezo wake, chini ya kivuli cha imani na matendo mema, na katika kukabiliana na mabeberu waovu, linaweza kusimama kidete na kutoa wito wa maadili ya Kiislamu kwa ulimwengu kwa sauti kubwa zaidi kuliko hapo awali.
Amesisitiza kwamba huzuni kubwa ya kuuawa wanasayansi kadhaa, makamanda wa jeshi na raia wengine haijaweza na haitaweza kuwasimamisha vijana wa Iran wenye hima kubwa, akibainisha kwamba familia za mashahidi hawa zenyewe ziko mstari wa mbele katika harakati hiyo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa sababu kuu ya mkanganyiko wa mataifa ya kibeberu si mpango wa nyuklia wa Iran, bali ni msimamo wa nchi hii dhidi ya utaratibu usio wa kiadilifu na wa kiimla wa kimataifa na hatua yake ya kuanzisha mfumo wa kitaifa na kimataifa wenye haki.
Amewasihi wanafunzi walio nje ya nchi kutambua uwezo wao, kumkabidhi Mungu nyoyo zao na kuongoza vyama vya wanafunzi kuelekea kwenye harakati hiyo.
Mnamo Juni 13, Marekani na Israel zilianzisha vita dhidi ya Iran na kuwaua makamanda kadhaa wa ngazi za juu, wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida.
Vikosi vya Jeshi la Iran vilijibu mashambulizi hayo kwa kulenga vituo vya kimkakati katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu na Israel pamoja na kambi ya jeshi la Marekani ya al-Udeid huko Qatar, ambayo ndiyo kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Magharibi ma Asia.