Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imeiamuru Kampuni ya M/S Climate Consult (T) Limited kulipa zaidi ya Sh146.6 milioni, baada ya kushindwa kutekeleza mkataba wa kusambaza vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mahakama imeeleza mwaka 2020 kampuni hiyo ilishinda zabuni ya kusambaza vifaa vya Tehama, zikiwamo kompyuta na printa kwa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo. Zabuni hiyo ilikuwa na thamani ya zaidi ya Sh708.2 milioni.

Katika shauri hilo la madai namba 32619/2024 wadai walikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya kampuni hiyo.

Hukumu ya shauri hilo ilitolewa Desemba 19, 2025 na Jaji Awamu Mbagwa, aliyelisikiliza na nakala yake kuwekwa kwenye tovuti ya mahakama.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, amesema kati ya fedha hizo Sh141.6 milioni ni ambazo kampuni hiyo ilipewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya utekelezaji wa zabuni.

Nyingine Sh5 milioni ni fidia kutokana na kushindwa kutekeleza makubaliano. Mahakama imeamuru kampuni hiyo kulipa riba kiasi kilichopunguzwa cha asilimia saba kuanzia tarehe ya hukumu hadi pale malipo yote yatakapokamilika pamoja na kulipa gharama zote za kesi.

Chanzo cha shauri

Chanzo cha mgogoro huo ni madai ya uvunjwaji wa hati ya makubaliano kati ya mdai wa kwanza na mdaiwa Novemba 30, 2023.

Kampuni hiyo inadaiwa ilikiuka masharti ya mkataba na kushindwa kumjerejeshea mdai wa kwanza zaidi ya Sh141.6 milioni.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mwaka 2020 kampuni hiyo ilishinda zabuni yenye thamani ya Sh708.2 milioni ili kusambaza vifaa vya Tehama katika taasisi zilizo chini ya mdai wa kwanza. Mdai wa kwanza na kampuni hiyo waliingia mkataba Aprili 20, 2020.

Ilielezwa mahakamani kuwa, mkataba huo ulikuwa wa usambazaji wa vifaa hivyo chini ya mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP).

Kwa mujibu wa mkataba, kabla ya kuanza kazi, kampuni ililipwa malipo ya awali ya Sh141.6 milioni ili iweze kuandaa na kusambaza vifaa hivyo.

Hata hivyo, licha ya kupokea fedha hizo, ilishindwa kuwasilisha vifaa kama ilivyokubaliwa.

Wizara iliipa kampuni hiyo muda wa ziada mara kadhaa ili iweze kutimiza wajibu wake, lakini juhudi zote zilishindikana. Baadaye ililazimika kuanza mazungumzo ya amani kupitia Ofisi ya AG.

Mazungumzo hayo yalizaa matunda, Novemba 30, 2023 pande zote mbili zilisaini hati ya makubaliano ya suluhu.

Katika makubaliano hayo kampuni hiyo ilikubali kurejesha fedha zote ilizopokea ndani ya siku 75 kuanzia tarehe ya kusaini makubaliano hayo.

Hata hivyo, ilielezwa mahakamani kuwa, kampuni hiyo haikutekeleza makubaliano hayo, kwani haikurejesha fedha ndani ya muda uliokubaliwa wala baada ya kutolewa kwa notisi kadhaa za kukumbushwa.

Kutokana na kukaidi makubaliano hayo, wizara iliamua kufungua kesi Mahakama Kuu kuomba haki itendeke.

Katika kesi hiyo, iliomba mahakama iiamuru kampuni hiyo ilipe Sh141.6 milioni, riba kwa kiwango cha asilimia 27 kuanzia tarehe ya uvunjaji mkataba na kushindwa kulipa hadi tarehe nyingine.

Mengine ni riba kwa kiasi tajwa kwa kiwango cha asilimia saba kuanzia tarehe ya kutangazwa hukumu na amri ya mahakama hadi malipo kamili na ya mwisho yatakapofanyika, fidia ya jumla kwa uvunjaji wa makubaliano na mkataba wa zabuni, gharama za kesi na amri zingine ambazo mahakama itaona zinafaa kutolewa.

Revocatus Raymond, mmoja wa mashahidi wa wadai aliwasilisha mahakamani hati kadhaa, ikiwamo nakala iliyothibitishwa ya hati ya makubaliano kati ya kampuni hiyo na Wizara ya Elimu, Sayansi ya Teknolojia ya Novemba 30, 2023.

Nyingine ni barua kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kampuni hiyo ya Februari 23, 2024 na notisi ya siku 10 ya Aprili 24, 2024 kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenda kwa kampuni hiyo.

Katika utetezi wake, kampuni hiyo ilipinga madai hayo ikidai walilazimishwa kusaini hati ya suluhu.

Mdaiwa alikuwa na mashahidi wawili, akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Majaliwa Burhani, aliyekuwa shahidi wa kwanza.

Aliwasilisha mahakamani maombi ya dhamana ya malipo ya awali ya Aprili 22, 2020 namba CBAT/096/2020 na hati ya uwakilishi ya kawaida ya Novemba 15, 2019.

Katika ushahidi wake alisisitiza hakusaini hati ya makubaliano kwa hiari. Alipohojiwa alikiri kupokea kutoka kwa mdai wa kwanza Sh141.6 milioni lakini hakusambaza vifaa vyovyote.

Shahidi wa pili, George Mwalongo, ambaye kimsingi ushahidi wake ulihusu kusainiwa mkataba wa zabuni kwa ajili ya usambazaji wa vifaa hivyo na kuithibitishia mahakama kuwa alikuwa ameidhinishwa na kampuni hiyo kuingia mkataba.

Uamuzi Jaji

Jaji Mbagwa amesema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama inaangalia masuala matatu; iwapo mdaiwa alivunja hati ya suluhu ya Novemba 30, 2023, iwapo anadaiwa na mdai wa kwanza Sh141.6 milioni na nafuu gani ambazo pande husika zinastahili kupata.

Kuhusu hoja ya kwanza, amesema malalamiko ya kampuni hiyo kudai kulazimishwa kusaini makubaliano hayo, mahakama inakataa hoja hiyo kwani kampuni haikuleta ushahidi wowote kuthibitisha madai ya kulazimishwa.

Jaji Mbagwa amesema kwa mujibu wa sheria, makubaliano yanayosainiwa kwa hiari yanawafunga wahusika wote. Amesema mahakama haina mamlaka ya kubadilisha masharti ya makubaliano yaliyokubaliwa na pande husika.

Amesema kushindwa kwa kampuni hiyo kurejesha fedha ni uvunjaji wa wazi wa makubaliano.

“Baada ya kutathmini ushahidi wa pande zote mbili, mahakama inashikilia kwamba pande zote mbili zilisaini makubaliano kwa kuridhia, kwa hiyo zilifungwa na masharti ya hati ya makubaliano. Hivyo, mdaiwa alikiuka masharti ya makubaliano kwa kushindwa kurejesha fedha ndani ya siku 75 walizokubaliana,” amesema.

Hoja iwapo kampuni hiyo inadaiwa Sh141.6 milioni na mdai wa kwanza, mahakama imesema kufuatia majadiliano ya sababu ya kwanza, mdaiwa hapingi kupokea fedha hizo kama malipo ya awali yaliyokusudiwa kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya kimkataba, pia anakubali kutokusambaza vifaa hivyo.

“Kutokana na mdaiwa kushindwa kutekeleza mkataba wa usambazaji, waliingia katika hati ya makubaliano kuwa arudishe fedha alizopokea. Hata hivyo, ameshindwa kurejesha fedha hizo ni wazi kuwa anadaiwa na mdai wa kwanza,” amesema.

Jaji Mbagwa katika hoja ya tatu amesema ni kanuni ya sheria chini ya kifungu cha 73 cha Sheria ya Mkataba kuwa, upande unaovunja mkataba unawajibika kumlipa fidia mwingine, kwani amesababisha usumbufu kwa mdai wa kwanza.

Mahakama imehitimisha uamuzi kwa kuamuru kampuni hiyo kumlipa mdai wa kwanza Sh141.6 milioni, fidia ya Sh5 milioni na kulipa riba kwa kiasi kilichopunguzwa cha asilimia saba kuanzia tarehe ya hukumu hadi pale malipo yote yatakapokamilika pamoja na kulipa gharama zote za kesi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *