WAZIRI wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene ametoa mwito kwa Watanzania kulinda amani na kudumisha upendo, kwani vimeleta mwanga ili wanadamu waishi kwa furaha.
Simbachawene aliyasema hayo katika ibada ya Krismasi katika Kanisa Katoliki Parokia ya Pwaga wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
“Rai yangu kwa Watanzania wenzangu wote katika kuadhimisha Krismasi, napenda niseme amani na upendo, haki na mshikamano vimeleta nusuru, vimeleta mwanga ili wanadamu tuishi kwa furaha na matumaini kwamba siku moja tutakwenda kukutana na Baba (Mungu)…,” alisema.
Aliongeza: “Na tujue hapa duniani kila kitu ni ubatili, mali na vitu havitatufanya tuweze kuutukuza utukufu wa Mungu, bali maisha na ukweli wetu tunaoishi na wanadamu wenzetu, na upendo tunaooneshana sisi kwa sisi.”
Alisema maisha ya sasa uongo umekuwa mwingi ambao umekuzwa na uwepo wa teknolojia na kwamba yapo mambo ambayo nchi inapitia kipindi hiki haijawahi kushuhudiwa.
“Watu wamekuwa wabinafsi sana na hawana upendo, wanasingiziana wananeneana mabaya kiasi kwamba unakumbuka zile nyakati ngumu za maisha ya binadamu na kuona ni mambo kama yale yanarudia tena wakati huu,” alisema.
Alisisitiza: “Tunapoadhimisha kuzaliwa kwa Kristo, tumeambiwa kuwa Kristo ni asili ya haki, asili ya upendo, asili ya mshikamano, Kristo ni nusuru, Kristo ni mwanga. Haya yote yanaashiria ulimwengu… tunapaswa kuishi kwa upendo na kutambua kila mmoja ana haki katika maisha ya hapa ulimwenguni,” alisema.
Tangu Oktoba mwaka huu kumeibuka wimbi la watu, hasa vijana wanaofanya vurugu kwa madai ya kutaka haki, huku wengine wakiharibu miundombinu na mali za serikali na watu binafsi.
Taarifa ya Jeshi la Polisi jana imesema nchi ni shwari na Watanzania walisherehekea Sikukuu ya Krismasi bila bugudha yoyote.
Msemaji wa Polisi, David Misime alisema kwenye taarifa kuwa wananchi waendelee na shughuli zao za kujenga taifa, kwani hakuna tishio lolote la kuvurugika kwa amani.
“Jeshi la Polisi tunatoa shukurani kwa wananchi kwa kulinda amani katika kipindi chote cha kabla, wakati na baada ya Sikukuu ya Krismasi, tunawahakikishia nchi iko salama,” alisema.
