
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kwamba Marekani inafuata “sheria ya mwituni” badalaya ya diplomasia, ikitumia nguvu na vikwazo ili kuendeleza maslahi yake.
Araqchi alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia wanafunzi na wasomi katika Chuo Kikuu cha MGIMO cha Russia wiki iliyopita. Matamshi yake yametolewa leo na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Katika hotuba yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisisitiza kwamba “kwa masikitiko makubwa mfumo wa kimataifa unaelekea kwenye shaghalabaghala”.
“Baada ya kuanzishwa Umoja wa Mataifa, nchi mbalimbali zilijaribu kuunda utaratibu unaozingatia sheria na kanuni za kimataifa, lakini tunachoshuhudia leo, hasa katika sera mpya za serikali ya Marekani, ni kupuuzwa sheria na kuwekwa mahali pale matumizi ya nguvu na mabavu,” amesema Araqchi.
Mwanadiplomasia mkuu wa Iran ameongeza kuwa sera ya kigeni ya Rais wa Marekani, Donald Trump, inategemea “amani kupitia mabavu”, wakati ubinadamu ukijaribu kwa miaka mingi kupata amani kupitia diplomasia na sheria.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema: “Amani kupitia mabavu ina maana kwamba yeyote aliye na nguvu kubwa zaidi huwalazimisha wengine matakwa yake; hii ndiyo ‘sheria ya mwituni’.”
Sayyid Abbas Araqchi amesema kwamba Washington sio tu kwamba “inaingilia kati popote duniani, inafanya mashambulizi, mauaji na kuweka vikwazo”, lakini pia inampa mshirika wake huko Asia Magharibi, yaani Israel, ruhusa ya “kufanya atakalo kinyume na sheria zote za kimataifa.”