
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema shirika hilo limefanikiwa kupeleka ujumbe wa tathmini huko El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya UN imeeleza kwamba kutumwa ujumbe wa kutathmini hali huko El Fasher kunafuatia majadiliano magumu yenye malengo ya kibinadamu, ikisisitiza kwamba huo ni ujumbe wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuwasili katika mji huo ambao umezingirwa kwa muda mrefu, na kushuhudia mapigano makali na vitendo vya ukatili dhidi ya raia na wafanyakazi wa huduma za kibinadamu.
Inafaa kuashiria hapa kwamba wapiganaji wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) waliuzingira mji wa El Fasher kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, na kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya wakazi wake baada ya kuudhibiti.
Gavana wa Jimbo la Darfur nchini Sudan, Minni Arko Minnawi, ameviambia vyombo vya habari kuwa, katika kipindi cha siku tatu tu Wasudan 27,000 waliuliwa na wapiganaji wa RSF wakati wanamgambo wa vikosi hivyo walipoendeleza wimbi la mauaji baada ya kuuteka mji wa el-Fasher mwishoni mwa mwezi uliopita.
Hapo awali, maafisa na wafanyakazi wa utoaji misaada ya kibinadamu walikadiria idadi ya vifo kuwa ni zaidi ya watu 2,500.