Uamuzi wa kuitambua Somaliland kama taifa huru ulitangazwa na serikali ya Israel jana Ijumaa, hatua ambayo imezua upinzani mkubwa kimataifa.

Somaliland, eneo lenye Waislamu wengi kaskazini mwa Somalia na lenye idadi ya watu wapatao milioni tano, limekuwa likiendesha shughuli zake za kiserikali kama taifa huru kwa zaidi ya miongo mitatu bila kutambuliwa rasmi.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed Abdullahi walisaini tamko la pamoja la kuthibitisha utambuzi huo, ambao Israel ilisema umefanywa kwa kuzingatia kile walichokiita “roho ya Mkataba wa Abraham.” Kulingana na taarifa, Netanyahu alimualika Rais wa Somaliland kwa ziara rasmi nchini Israel.

Mkataba wa Abraham, ulioanzishwa na Rais wa Marekani Donald Trump mnamo mwaka 2020, hapo awali ulipelekea mataifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Morocco na Sudan kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel.

Nchi nyingine, ikiwemo Ethiopia ambayo ni jirani na Somalia, Umoja wa Falme za Kiarabu pia zina mahusiano na Somaliland lakini hazijaitambua rasmi kama taifa huru.

Ukosoaji wa kimataifa

Hatua ya kuitambua Somaliland imezua hasira miongoni mwa mataifa kadhaa ya kikanda.

Serikali ya Somalia imelaani hatua ya Israel kuitambua Somaliland kama nchi huru, ikisema ni shambulio la makusudi na kinyume cha sheria dhidi ya mamlaka ya nchi. Somaliland ni sehemu “isiyotenganishwa” ya ardhi ya Somalia, imeongeza.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit, pia ameikosoa Israel, akisema hatua hiyo ni “ukiukaji wazi wa sheria za kimataifa” na kupuuza misingi ya umoja wa eneo na mamlaka ya kitaifa.

Umoja wa Afrika unaowakilisha mataifa yote 55 ya Afrika yanayotambuliwa kimataifa, umeonya kuwa jaribio lolote la kudhoofisha umoja, mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya Somalia linaweza kuweka kile walichokiita “mfano hatari wenye athari kubwa kwa amani na uthabiti kote barani.”

Kulingana na kituo cha televisheni cha Israel, Channel 12, mawasiliano ya siri kati ya Israel na Somaliland yalianza miezi kadhaa iliyopita. Wakati huo, Israel ilikuwa ikitafuta nchi zinazoweza kupokea wakaazi katika Ukanda wa Gaza uliokumbwa na vita.

Somaliland | Addis Abeba 2025 | Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed
Ziara ya Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed Abdullahi nchini EthiopiaPicha: Ministry of Foreign affairs of Somaliland

Mshirika wa karibu wa Netanyahu, Rais wa Marekani Donald Trump, hapo awali aliweka wazi mpango wa kuwahamisha wakaazi wa Gaza, jambo lililozua ukosoaji wa kimataifa.

Sababu nyingine kuu ya Israel kujihusisha na Somaliland, kwa mujibu wa gazeti la Times of Israel, ni ukaribu wa eneo hilo na Yemen.

Upatikanaji wa ardhi na anga ya Somaliland ungeisaidia Israel kufuatilia kwa urahisi zaidi shughuli za waasi wa Houthi na hata ikibidi, kushambulia wanamgambo hao wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen.

Wanamgambo wa Houthi wamekuwa wakizishambulia meli za kibiashara zinazodhaniwa kuwa na uhusiano na Israel katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.

Mashambulizi hayo yameongezeka tangu kuanza kwa mgogoro wa Gaza, na yameathiri usalama wa njia za biashara ya kimataifa, hususan usafirishaji kupitia Bandari ya Bab el-Mandeb—njia muhimu inayounganisha Bahari ya Shamu na Bahari ya Hindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *