
China imeyawekea vikwazo makampuni 20 ya ulinzi ya Marekani na watendaji wake 10 wakuu kutokana na shehena kubwa zaidi ya mauzo ya silaha za Marekani kwa Taiwan.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imetangaza vikwazo dhidi ya makampuni kadhaa ya Marekani likiwemo tawi la Boeing la St. Louis, Northrop Grumman Systems na L-3 Harris Marine Services, pamoja na watendaji 10 wakuu wa Marekani katika makampuni hayo.
Hatua hiyo ya China, inazuilia mali zote za makampuni hayo na watu binafsi zilizoko nchini China na kuzuia mashirika na watu binafsi wa ndani kufanyakazi na makampuni hayo ya Marekani.
Uamuzi huo wa China pia unawapiga marufuku watu binafsi walio kwenye orodha ya vikwazo, akiwemo mwanzilishi wa kampuni ya ulinzi ya Andorel na watendaji wakuu tisa wa kampuni zilizowekewa vikwazo, kuingia nchini China.
Marekani imepinga uamuzi huo wa China.
Hatua hiyo ya China imekuja baada ya Washington kutangaza wiki iliyopita mkataba wa mauzo ya silaha wenye thamani ya dola bilioni 11.1 kwa Taiwan. Mkataba huo unatambuliwa kuwa mkubwa zaidi wa silaha kuwahi kutiwa saini baina ya Washington na Taiwan, jambo ambalo limeikasirisha Beijing.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema katika taarifa yake siku ya Ijumaa kwamba “suala la Taiwan ni muhimu kwa maslahi makuu ya China na ndio mstari wa kwanza mwekundu ambao haupaswi kuvukwa katika uhusiano kati ya Washington na Beijing.”
Aliongeza kwamba “vitendo vyovyote vya uchochezi vinavyovuka mipaka myekundu kuhusu suala la Taiwan vitakabiliwa na jibu kali kutoka China,” na ametoa wito kwa Washington kusitisha juhudi zake “hatari” za kukipatia silaha kisiwa hicho.
China inaitambua Taiwan kuwa sehemu ya ardhi yake, jambo ambalo linapingwa na Taipei.