UONGOZI wa Mtibwa Sugar umesema hautakurupuka kufanya usajili katika dirisha dogo, lakini moja ya nafasi zitakazofanyiwa kazi ni eneo la ushambuliaji ukilenga kushusha straika mmoja wa kimataifa anayejua kufunga mabao ili kuwaondolea hali tete waliyonayo kwa sasa katika Ligi Kuu Bara.

Mapema katika gazeti la jana kocha wa timu hiyo, Yusuf Chipo alinukuliwa akidai kuhitaji straika akiwamo mzawa, lakini mabosi wa klabu hiyo wameweka wazi kwamba wanalifanyia kazi ombi la Mkenya huyo la kuletewa mashine ya maana kumaliza ukame wa mabao kikosini.

Hadi ligi inasimama kupisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, Mtibwa imecheza mechi nane ikifunga mabao manne na kufungwa pia manne, ikivuna pointi 10 ikishika nafasi ya saba, kitu kinachowafanya mabosi wa timu hiyo chini ya kocha Yusuf Chipo kutaka kulitumia dirisha dogo kufanya usajili uatakaowabeba Ligi Kuu ikirudi Januari 21, mwakani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Swabri Aboubakar amesema wanasubiri ripoti kutoka kwa kocha ambayo itawafikia siku tano zijazo ili waweze kufanyia kazi maeneo ambayo wanaamini yameonyesha udhaifu katika mechi walizocheza huku akilitaja eneo la ushambuliaji.

“Kabla ya ripoti kama viongozi tumeona pengo eneo la ushambuliaji na tayari tumeanza mchakato wa kutafuta mshambuliaji wa maana ambaye atasaidiana na wachezaji waliopo, na mchezaji katika eneo hilo tunataka kuwa nyota wa kigeni. Hatutaki kukurukpuka kusajili ilimradi,” amesema Swabri na kuongeza:

“Dirisha dogo sio rahisi kupata mchezaji bora wengi wanakuwa na mikataba na timu zao, hivyo tunahitaji jicho la kocha kwwenye mapendekezo ili tupate mchezaji mwenye ubora unaotakiwa. Tunafahamu haitakuwa rahisi, lakini imani ni kupata mchezaji mzuri.”

Swabri amesema mara baada ya kupokea ripoti ya kocha wataweka wazi ni nafasi gani nyingine zinatakiwa kufanyiwa kazi mara baada ya dirisha dogo kufunguliwa mapema mwezi ujao, huku akisisiriza kuwa wataongeza umakini kwenye usajili ili kuboresha kikosi chao.

“Hatutaki kurudi tulipotoka Ligi Kuu ni ngumu mechi chache tulizocheza zimetusanua na kutufanya tuwekeze nguvu zaidi kwenye usajili wa dirisha lijalo ili tuweze kuendana na kasi iliyopo, hilo tunaamini linawezekana kama tutafanya usajili kwa mahitaji ya benchi la ufundi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *