
WAKATI leo Desemba 28, 2025 michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inafunguliwa kwenye Uwanja wa New Aman Complex uliopo Unguja, itapigwa mechi moja pekee badala ya mbili kama ilivyopangwa awali, huku sababu za kufanya hivyo ikitajwa
Ratiba ya awali ilionyesha saa 10:15 jioni, Mlandege itacheza na Singida Black Stars, kisha saa 2:15 usiku ni zamu ya Azam dhidi ya URA kutoka Uganda.
Mabadiliko ya ratiba hiyo yamebadilika na sasa leo itapigwa mechi moja kati ya Mlandege dhidi ya Singida Black Stars kuanzia saa 1:00 usiku.
Katibu wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026, Rashid Said Suleiman, ameiambia Mwanaspoti kuwa sababu za kuahirisha mechi ya Azam dhidi ya URA ni kutokana na changamoto waliyoipata wakali hao kutoka Uganda.
“Ni kweli mwanzo tulisema siku ya ufunguzi kutakuwa na mechi mbili, lakini kuna mabadiliko yamefanyika na sasa itachezwa mechi moja ya Mlandege dhidi ya Singida.
“Ndugu zetu URA walipata changamoto kidogo, hivyo wamechelewa kufika, tunatarajia leo watakuwa hapa Unguja, tukaona si busara wafike na wacheze mechi.
“Uamuzi tulioufanya ni kuisogeza mbele mechi hiyo na sasa tunaangalia tuipangie siku ya kuchezwa ili kuendana na ratiba ilivyo,” amesema Suleiman.