Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti kuwa watu zaidi ya 200, wakiwemo wanawake na watoto wameuawa katika mashambulizi ya kikabila yaliyofanywa na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) huko Darfur nchini Sudan.

Mtandao huo wa Madaktari wa Sudan umewanukuu manusura wa mauaji hayo waliofika katika kambi za wakimbizi huko Tina, karibu na mpaka wa Sudan na Chad, na kuripoti kuwa raia walishambuliwa na kuuawa kwa misingi ya kikabila katika maeneo ya Ambro na Abu Qamra huko Darfur Kaskazini na Sirba huko Darfur Magharibi baada ya wanamgambo wa RSF kushambulia maeneo hayo.

“Wahanga ni pamoja na watoto wadogo, wanawake na wanaume ambao walilengwa kwa makusudi na kuuliwa kwa misingi ya kikabila’ imesema taarifa hiyo, ikielezea mashambulizi hayo kama ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na haki za binadamu. 

Mauaji haya yameripotiwa huku mapigano makali yakiendelea huko Darfur Kaskazini.

Duru za ndani ya Sudan zimearifu kuwa wanamgambo wa RSF Jumatano iliyopita walishambulia maeneo ya Abu Qamra na na Ambro na kudai kuyadhibiti maeneo hayo mawili.

Maelfu ya watu wameuliwa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi kufuatia mapigano yaliyoanza Sudan mwezi Aprili 2023 kati ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo wa RSF.

Waziri Mkuu wa Sudan, Kamil Idris, Jumatatu iliyopita alihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuwasilisha mpango ambao unajumuisha usitishaji mapigano kamili chini ya usimamizi wa kikanda na kimataifa, akisisitiza kwamba Sudan imelipa gharama kubwa kutokana na mzozo unaoendelea nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *