Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wameelekea kwenye masanduku ya kura katika zoezi la uchaguzi mkuu huku Rais Archange Touadéra akiwania kiti cha urais kwa muhula wa tatu.

Archange Touadéra mwaka 2023 alifanya marekebisho ya katiba yaliyoondoa ukomo wa mihula ya urais. 

Hatua hiyo ilikosolewa pakubwa na kuibua maandamano ya wapinzani waliomtuhumu kuwa ana lengo la kubakia madarakani milele. 

Mrengo wa upinzani una wagombea sita wanaoongozwa na mawaziri wakuu wawili wa zamani, Anicet-Georges Dologuele na Henri-Marie Dondra.

Wanasiasa hao wawili walinusurika jaribio la wafuasi wa Touadéra waliotaka wasiruhusiwe kugombea kiti cha rais kwa madai kuwa wana uraia wa kigeni.

Pamoja na hayo, Touadera anatazamiwa kuibuka mshindi katika uchaguzi wa urais wa leo kwa kuzingatia namna alivyosimamia taasisi za serikali na vyanzo vya mapato vya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais yanatazamiwa kutangazwa tarehe 5 Januari. Duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati itafanyika mwezi Februari 2026 iwapo hakutakuwa na mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, na uchaguzi wa marudio wa wabunge utafanyika Aprili 5, 2026. 

Weledi wa masuala ya siasa wametahadharisha kuhusu machafuko na ghasia baada ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kuzingatia uwezekano wa wapinzani kupinga ushindi wa Archange Touadera. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *