KOCHA Mkuu wa Gunners ya jijini Dodoma, Juma Ikaba, amesema kwa sasa wanapambana kuwaingiza wachezaji wapya tisa katika mfumo pindi dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Januari Mosi 2026, baada ya kushindwa kucheza tangu msimu umeanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ikaba amesema kuna wachezaji tisa ambao hawajaichezea timu hiyo hadi sasa, baada ya baadhi yao kukosea kuingiza majina kwa usahihi katika mfumo, jambo lililosababisha kushindwa kupata leseni ya kucheza mapema.

“Wachezaji wengi walikuwa wanaingiza majina yao kwa mazoea sasa ilipokuja katika mfumo ili kuwathibitisha ikaleta shida na mwishoni kushindwa kucheza, tutakachokifanya dirisha hili ni kupambania hilo ili waungane na wenzao,” amesema Ikaba.

Gunners imepanda Ligi ya Championship msimu huu, baada ya kuongoza First League kundi B na pointi 35, kufuatia kushinda mechi 11, sare mbili na kupoteza moja, ikiungana na kikosi cha Hausung kutoka Njombe iliyoongoza kundi A na pointi 25.

Baada ya timu hizo kuongoza makundi yao na kupanda Championship, zilicheza mechi ya fainali kusaka bingwa mpya wa First League kwa msimu wa 2024-2025, ambapo kikosi hicho cha Gunners kilitwaa ubingwa huo kufuatia kuifunga Hausung mabao 3-0.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *