
Vikosi vya usalama vya Syria vimewaua watu wawili leo Jumapili, Desemba 28, huku vikitawanya maandamano ya Alawite katika eneo la pwani, kulingana na Shirika la Haki za Binadamu nchini Syria (SOHR), shirika lisilo la kiserikali lenye mtandao mkubwa wa vyanzo nchini. Hospitali katika eneo hilo imepokea miili miwili, chanzo cha hospitali kimeliambia shirika la habari la AFP.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mamlaka haijathibitisha kuwafyatulia risasi waandamanaji, lakini imesema “wamedhibiti hali hiyo” na kuwashutumu wafuasi wa Rais wa zamani Bashar Al Assad kwa kushambulia vikosi vya usalama.
Maelfu ya Waalawi wa Syria wameandamana katika miji kadhaa, wakidai kusitishwa kwa vurugu kufuatia shambulio baya dhidi ya msikiti wa jamii hii ya Waislamu wachache. Mkutano wa hadhara ulifanyika katika kitongoji cha Wadi al-Dahab cha Homs, ambapo shambulio lilitokea siku ya Ijumaa wakati wa sala, na kuua watu wanane.
Waalawi, tawi la Uislamu wa Kishia ambalo Rais aliyeondolewa madarakani Bashar Al Assad anatoka, wamekuwa wakilengwa na mashambulizi tangu muungano wa Kiislamu ulipochukua madaraka huko Damascus mwishoni mwa mwaka 2024. Maandamano hayo yaligubikwa na makabiliano na wafuasi wa utawala huko Homs na pia katika mji wa pwani wa Latakia, mwandishi wa shirka la habari la AFP ameripoti, akibainisha kuwa milio ya risasi ilisikika.
Shirika la Haki za Binadamu la Syria (SOHR), shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake Uingereza lenye mtandao mkubwa wa vyanzo nchini Syria, limeripoti watu kadhaa kujeruhiwa. “Assad ameondoka, na hatumuungi mkono Assad … Kwa nini mauaji haya?” anauliza Numeir Ramadan, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 48. “Kwa nini mashambulizi haya ya yanafanyika, bila kizuizi chochote, uwajibikaji, au usimamizi?” anaongeza. Ghazal Ghazal, rais wa Baraza la Kiislamu la Alawite nchini Syria na Nje ya nchi, alitoa wito siku ya Jumamosi “kuonyesha ulimwengu kwamba jamii ya Alawite haiwezi kudhalilishwa au kutengwa.” “Hatutaki vita vya wenyewe kwa wenyewe; tunataka shirikisho la kisiasa. Hatutaki ugaidi wenu. Tunataka kuamua hatima yetu wenyewe,” alisema katika ujumbe wa video uliorushwa kwenye Facebook.
Uso wake ulionekana Jumapili katika picha zilizowekwa juu na umati, ambao uliimba kaulimbiu zinazotaka uhuru zaidi. “Mahitaji yetu ya kwanza ni shirikisho kukomesha umwagaji damu.” “Wanatuua kwa sababu sisi ni Waalawi,” analalamika Hadil Saleh, mama mwenye umri wa miaka 40.
Saraya Ansar al-Sunna, kundi la Sunni lisilojulikana sana, lilidai kuhusika na shambulio la Ijumaa kwenye Telegram, likiapa kuendelea na mashambulizi yanayowalenga “makafiri na waasi.” Mnamo mwezi Machi, mauaji ya halaiki kwenye pwani yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,700, wengi wao wakiwa Waalawi, baada ya mapigano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa Bashar Al Assad, kulingana na Shirika la Haki za Binadamu la Syria (SOHR). Tume ya kitaifa ya uchunguzi ilihesabu angalau watu 1,426 walifariki, wengi wao wakiwa raia.
Maelfu ya watu waliandamana mwishoni mwa mwezi Novemba katika miji kadhaa kando ya pwani ya Syria kulaani vurugu dhidi ya Waalawi, ambao wana uwepo mkubwa katika eneo hilo. Siku ya Jumapili, waandamanaji pia wamedai kuachiliwa kwa wafungwa kutoka jamii ya Waalawi. Kulingana na televisheni ya serikali ya Syria, 70 kati yao waliachiliwa siku mbili zilizopita “baada ya kuthibitishwa kwamba hawakuhusika katika uhalifu wa kivita,” na watu zaidi wanatarajiwa kunatarajiwa.