China, katika ukosoaji ulio wazi dhidi ya Marekani, imetangaza kuwa Washington, kwa ajili ya kulinda ubabe wake wa kijeshi, inajihusisha na mbinu za kutia fitna, kugawa na kutawala.

Lin Jian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, katika mkutano wa habari wa Alhamisi tarehe 25 Desemba, akijibu ripoti mpya ya Wizara ya Vita ya Marekani kuhusu kupungua kwa mvutano wa mpakani kati ya Beijing na New Delhi na uwezekano wa kuzuia kuimarika kwa uhusiano wa Marekani na India, alisisitiza kuwa Washington, kwa ajili ya kulinda ubabe wake wa kijeshi, inajihusisha na mbinu za kutia fitna na kugawa. Amesisitiza kuwa: ripoti mpya ya Wizara ya Vita ya Marekani imepotosha sera ya ulinzi ya Beijing na inalenga kuchochea mgawanyiko kati ya China na mataifa mengine.”

Matamshi haya yalitolewa wakati Pentagon katika ripoti moja ilidai kuwa Beijing huenda ikatumia kupungua kwa mvutano katika mpaka na India ili kuzuia kuimarika kwa uhusiano kati ya Washington na New Delhi. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, amesisitiza kuwa Marekani kwa ajili ya kulinda ubabe wake wa kijeshi inatafuta visingizio vya kuvuruga mambo na China inapinga vikali sera hiyo.

Mwanadiplomasia huyu wa China aliendelea kusisitiza kuwa Beijing daima huangalia uhusiano wake na India kwa mtazamo wa kimkakati na wa muda mrefu, na inataka pamoja na New Delhi kupitia kuimarisha mawasiliano, kuongeza imani ya pande zote, kupanua ushirikiano na kusimamia ipasavyo tofauti zilizopo, kuendeleza uhusiano wa pande mbili katika njia yenye afya na thabiti. Lin Jian, akisisitiza kuwa hali ya mipaka ya China na India kwa ujumla ni thabiti na njia za mawasiliano kati ya pande mbili ziko wazi na zinafanya kazi, alibainisha kuwa tunapinga nchi nyingine kuingilia suala hili.

Ukosoaji wa hivi karibuni wa China dhidi ya Marekani, katika kujibu ripoti ya Pentagon, kwa mara nyingine umeonyesha kuwa Washington, kwa ajili ya kulinda ubabe wake wa kijeshi na kisiasa katika Asia, inajihusisha na siasa za kugawa kati ya nguvu za kikanda. Ripoti ya Pentagon ilidai kuwa China, kwa kupunguza mvutano wa mpakani na India, inalenga kuzuia kuimarika kwa uhusiano wa New Delhi na Washington. China imeita dai hili kuwa ‘lisilo na uwajibikaji’ na kusisitiza kuwa uhusiano wake na India unafuatwa kwa mtazamo wa kimkakati na wa muda mrefu.

Sababu za upinzani wa Marekani dhidi ya kuboreshwa kwa uhusiano wa China na India zinaweza kuchunguzwa katika mihimili kadhaa.

Kwanza, Marekani katika miaka ya hivi karibuni imejaribu kuitumia India kama uzani dhidi ya China ndani ya mkakati wa ‘Indo-Pasifiki’. Ukuruba wa India na China unadhoofisha mkakati huu na unasababisha kupungua kwa ufanisi wa miungano ya Washington katika eneo hilo.

Pili, Marekani ina wasiwasi kwamba utatuzi wa migogoro ya mipaka kati ya nchi hizi mbili unaweza kuwa msingi wa ushirikiano mpana zaidi wa kiuchumi na kiusalama. Ushirikiano wa aina hiyo unaweza kusababisha Marekani idhoofike katika masoko ya Asia na katika mlingano wa kiusalama za kikanda. Tatu, Washington ina hofu kwamba uhusiano wa karibu zaidi kati ya Beijing na New Delhi unaweza kuiondoa India katika ushiriki wa moja kwa moja katika miungano ya kupinga China kama QUAD, na kubadilisha mizani ya nguvu za kikanda kwa manufaa ya China.

Kwa upande mwingine, athari za kuongezeka kwa kiwango cha uhusiano kati ya China na India na utatuzi wa migogoro ya pande mbili juu ya uhusiano wa India na Marekani ni za kuzingatiwa sana. Ikiwa nchi hizi mbili zitaweza kusimamia migogoro ya mipaka na kuongeza imani ya pande zote, India haitahitaji tena kutegemea Marekani pekee kama mshirika wa kimkakati. Jambo hili linaweza kusababisha kupungua kwa utegemezi wa India kwa Washington katika nyanja za kijeshi na kiteknolojia. Aidha, ushirikiano mpana zaidi wa kiuchumi kati ya China na India, hususan katika sekta ya biashara na uwekezaji, utadhoofisha nafasi ya Marekani katika uchumi wa India.

Katika kiwango cha kijiografia ya siasa, ukuruba wa China na India unaweza kubadilisha mlingano wa nguvu za kisiasa, kiuchumi na kijeshi katika bara Asia. India ambayo hadi sasa imekuwa ikijulikana kama mshirika muhimu wa Marekani katika kudhibiti China, huenda ikasogea kuelekea sera ya mambo ya nje yenye uwiano zaidi. Sera ya aina hiyo itamaanisha kupungua kwa hamu ya India kushiriki katika miradi ya kiusalama chini ya uongozi wa Marekani. Matokeo yake, Washington itapoteza sehemu ya ushawishi wake katika Asia Kusini. Zaidi ya hayo, utatuzi wa migogoro kati ya China na India unaweza kuimarisha mashirika ya kikanda kama BRICS na Shirika la Ushirikiano la Shanghai, mashirika ambayo Marekani haina nafasi ndani yake na huzitazama kutoka nje.

Bila shaka, inapaswa kuzingatiwa kuwa uhusiano wa India na Marekani haujibani tu katika suala la China. New Delhi bado inahitaji teknolojia za hali ya juu na uwekezaji wa Kimarekani na ina ushirikiano mpana na Washington katika nyanja za ulinzi na nishati. Hata hivyo, iwapo uhusiano wa China na India utafikia kiwango cha kudumu na cha kimkakati, India itaweza kwa kujiamini zaidi kufuata sera ya ‘ujumuishaji wa pande nyingi’ na kupunguza utegemezi wake uliokithiri kwa Marekani. Jambo hili litamaanisha kupungua kwa nguvu ya Marekani ya kujadiliana katika mahusiano yake na New Delhi.

Wakati huohuo, upinzani wa Marekani dhidi ya kuboreshwa kwa uhusiano wa China na India unatokana na wasiwasi wa kimkakati na kijiografia ya siasa. Washington inajua kuwa ukuruba wa nguvu hizi mbili za Asia unaweza kubadilisha mizani ya kikanda na kudhoofisha nafasi ya Marekani katika Asia. Kwa upande mwingine, utatuzi wa migogoro na kuongezeka kwa kiwango cha ushirikiano kati ya China na India si tu kwamba utaathiri uhusiano wa India na Marekani, bali pia unaweza kusababisha kuundwa kwa utaratibu mpya katika Asia; utaratibu ambao ndani yake nguvu za kikanda zitakuwa na nafasi kubwa zaidi na haja ya kuingilia kwa Marekani itapungua.

Mabadiliko haya yanaonyesha kuwa mustakabali wa uhusiano wa kimataifa katika Asia unategemea zaidi kuliko wakati wowote ule juu ya maingiliano kati ya nguvu za kikanda. Ikiwa China na India zitaweza kuweka kando migogoro yao na kupanua ushirikiano wa kimkakati, Marekani italazimika kufanya upya tathmini ya sera zake na kutoka katika mtazamo wa kugawa kuelekea ushirikiano wa kweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *