Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza imetangaza kuwa, Angola na Namibia zimekubali kuruhusu kurejeshwa katika nchi hizo wahamiaji wasio rasmi na wahalifu baada ya serikali ya Uingereza kutishia kutoa adhabu ya vikwazo vya viza kwa nchi zinazokataa kutoa ushirikiano.

Taarifa ya wizara hiyo imesema, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeondolewa huduma za viza za haraka na matibabu ya upendeleo kwa viongozi na wapitishaji maamuzi baada ya kushindwa kukidhi vigezo vya Uingereza vya kuboresha ushirikiano.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Shabana Mahmood amesema, nchi hiyo inaweza kushadidisha hatua hadi kiwango cha kusitisha kabisa utoaji viza kwa DRC isipokuwa kama utoaji ‘ushirikiano utaimarika haraka’.

‘Tunatarajia nchi zichukue hatua kwa mujibu wa sheria. Ikiwa mmoja wa raia wao hana haki ya kuwepo hapa, lazima wamrejeshe,’ ameongezea kusema Mahmoud.

Makubaliano hayo yanaashiria mabadiliko makubwa ya kwanza chini ya mageuzi yaliyotangazwa mwezi uliopita, ambayo yanakusudia kufanya hadhi ya wakimbizi kuwa ya muda na kuharakisha kufukuzwa wale wanaowasili Uingereza kinyume cha sheria.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper amesema, nchi hiyo ‘imewaondoa zaidi ya watu 50,000 ambao hawana haki ya kukaa’ tangu Julai mwaka uliopita, likiwa ni ongezeko la asilimia 23 ikilinganishwa na kipindi kilichopita…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *